1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

231011 Euro Gipfel

24 Oktoba 2011

Matarajio ya mkutano wa viongozi wa nchi 17 zinazotumia sarafu ya Euro kwamba kungelipatikana suluhisho la madeni yamedidimia baada ya kubainika kwamba hatua ya pili ya mkutano inapaswa kuchukuliwa Jumatano ijayo.

https://p.dw.com/p/12xcg
Sarafu ya euro iko katika hali mbaya sana
Sarafu ya euro iko katika hali mbaya sanaPicha: picture-alliance/dpa

Kansela  wa  Ujerumani  Angela Merkel na Rais  Nicolas Sarkozy wa  Ufaransa walifanya  bidii ya kuonyesha umoja  kwenye mkutano  huo. Ujumbe uliowasilishwa na viongozi hao  ni msimamo wa pamoja katika kulitafuta suluhisho la mgogoro wa madeni. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaelekea kuwa wamepiga  hatua  katika juhudi zao za kuukabili mgogoro mkubwa wa madeni.

Katika  juhudi za kuepusha mfarakano, Rais Sarkozy amekiri kwamba amelazimika kurudi nyuma katika mabishano yake na Ujerumani juu  ya  jinsi ya kuchangia katika mfuko wa kuziokoa nchi zilizolemewa na madeni  katika Umoja wa Sarafu ya  Euro.

Hapo awali kiongozi huyo wa  Ufaransa alipendekeza kuugeuza Mfuko huo kuwa benki na kuiwezesha  wakati wote kukopa kutoka  Benki  Kuu ya Ulaya (ECB).

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha  la Kimataifa, Christine Lagard, wamesifu hatua nzuri iliyopigwa kwenye  mkutano huo.

Wazii Mkuu wa Poland, Donald Tusk, Kansela Angela Merkel na Rais wa Baraza wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy.
Wazii Mkuu wa Poland, Donald Tusk, Kansela Angela Merkel na Rais wa Baraza wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, marais na mawaziri  wakuu hawakufikia maamuzi thabiti kwenye mkutano wao wa  mjini Brussels.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amekiri kwamba hajui ni suluhisho lipi litakalokuwa mujarabu.

"Kwa usemi mwingine, miongoni mwa wataalamu wote waliokuwapo,  hakuna anayeweza kusema kwa uhakika njia  gani, ni sahihi kwa asilimia 100, kwa sababu tumeingia  katika mazingira tusiyoyajua. Kwa  sababu, hali kama hiyo katika Umoja wa Sarafu kama wa eneo la Euro, haijawahi kutokea." Amesema Kansela Merkel.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kutoa maelezo ya undani   zaidi kwenye mkutano wao mwingine utakaofanyika Jumatano ijayo.

Rais Sarkozy na Kansela Merkel wamesisitiza kwamba baina yao kwa jumla pana makubaliano.

Katika hatua nyingine ya juhudi za kuukabili mgogoro wa madeni, viongozi hao Ujerumani na Ufaransa waliwasilisha ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, kwamba ili masoko ya fedha yaanze tena kuzinunua dhamana na ili kurejesha hali ya uhakika katika eneo la Euro, Italia itapaswa ifanye mageuzi zaidi ya kiuchumi.

"Tunaendelea kuwa na imani na hisia za uwajibikaji wa wanaisasa, na  wanaopitisha maamuzi ya kifedha  na kiuchumi  nchini Italia." Amesema Rais Sarkozy.

Viongozi  wa  Umoja wa  Ulaya   wana wasiwasi huenda kiasi cha Euro bilioni 440 hakitatosheleza kwa ajili    ya kuiokoa nchi kubwa kama Italia. Hata hivyo, Rais wa Halmashauri Kuu  ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel  Barosso amesema kazi inaendelea kufanyika na  maamuzi yanatarajiwa kupitishwa Jumatano. Barroso amesema ana imani kwamba maamuzi hayo yatapitishwa.

Mwandishi: Riegert, Bernd/ZR Tafsiri: Abdu Mtullya Mhariri: Mohammed Khelef