1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy ataka mageuzi katika Umoja wa Ulaya

Abdu Said Mtullya2 Desemba 2011

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ametoa wito wa kuleta mageuzi kwenye Umoja wa Ulaya, kwa upande mmoja, na ndani ya nchi yake kwa upande mwengine akitaka pawepo hatua kali za udhibiti wa masuala ya fedha.

https://p.dw.com/p/13LAV
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: dapd

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesisitiza ulazima wa kuleta mageuzi nchini mwake na katika Umoja wa Ulaya kwa jumla.

Sarkozy amesema Umoja wa Sarafu ya Euro unahitaji udhibiti wa bajeti na utaratibu wa adhabu kwa nchi zinazokiuka nidhamu ya bajeti. Ameyasema hayo katika hotuba aliyoitoa mjini Toulon kwa watu 5,000 wanaomuunga mkono.

Kiongozi huyo wa Ufaransa pia ameeleza kuwa anakusudia kuujadili mpango wa pamoja wa Ufaransa na Ujerumani wa kuukabili mgogoro wa madeni, atakapokutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Paris jumatatu ijayo.

Mpango huo pia unahusu kuleta mabadiliko katika Mkataba wa Umoja wa Ulaya.

Sarkozy amesema yeye pamoja na Kansela Merkel watauwasilisha mpango huo kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo.

Rais Sarkozy pia amewataka wananchi wake wawe tayari kwa hatua za kubana matumizi katika sekta ya umma.