1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia na vita visivyo mwisho Yemen

Yusra Buwayhid
11 Novemba 2017

Huku Saudi Arabia ikiongeza nguvu katika mpaka wake dhaifu wa kusini, vita ilivyovianzisha Yemen vinaonekana kutodhibitika, waasi wanaendelea kudhibiti kaskazini na kinachotegemewa katika siku za mbele ni maafa.

https://p.dw.com/p/2nRWO
Jemen Luftangriff auf Saada
Picha: Reuters/N. Rahma

Licha ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia inayotaka kumrekesha rais aliyepo uhamishoni, na ambayo yameharibu sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, waasi wa madhehebu ya kishia, wanaooungwa mkono na Iran, bado wanadhibiti maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Sanaa.

Vita viliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 10,000 na kusababisha janga la njaa kwa mamilioni ya raia wa Yemen, havina dalili ya kumalizika katika siku za karibuni.

Waasi wa madhehebu ya Kishia wa watu wa jamii ya Houthi wanaonekana kudhibiti maeneo mengi na hasa kaskazini mwa nchi. Wanadhibiti taasisi za serikali, wana silaha za kutosha, na wanaungwa mkono pia na jeshi lenye nguvu lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh. Miundombinu kama vile huduma ya afya, maji na umeme hata hivyo imeharibika.

Wapinzani wao ni vikosi tiifu kwa rais aliyepo uhamishoni, Abed Rabbo Mansour Hadi, na mkusanyiko wa makabila tofauti yanayoongozwa na Saudi Arabia pamoja na mshirika wake mkuu, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Vikosi hivi kwa pamoja vinadhibiti kusini mwa Yemen, ikiwa ni pamoja na mji wa bandari wa Aden, wa pili kwa ukubwa na ngome ya serikali ya Hadi, lakini ni sehemu yenye usalama dhaifu, mivutano ya makundi na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yamepelekea kiongozi huyo kuuhama mji na kutokuwepo muda mwingi.

Vikosi vya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu havina nguvu ya kuidhibiti nchi nzima

Matokeo ya vita vya Yemen ni pamoja na kusambaa kwa utapiamlo na maradhi ya kuharisha kutokana na kubomolewa kwa miundombinu ya maji na matibabu.
Matokeo ya vita vya Yemen ni pamoja na kusambaa kwa utapiamlo na maradhi ya kuharisha kutokana na kubomolewa kwa miundombinu ya maji na matibabu.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Ingawa hatua inazochukua muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia za kufanya mashambulizi ya anga pamoja na kudhibiti usafiri wa majini haziwezi kuleta ushindi, lakini zimezuia uingiliaji kati wa kiwango kikubwa kutoka Iran. 

Iran kwa kiitikadi ipo karibu na waasi wa jamii ya Houthi na ipo tayari kuwapa uungwaji mkono wa kisiasa na kidiplomasia, lakini inakana kuwatumia silaha.

Mara kwa mara, silaha zinakamatwa zikiwa zinasafirishwa katika boti za kuvulia zikielekea nchini Yemen, na jeshi la majini la Marekani na vikosi vya muungano wa kijeshi vinaishutumu Iran kuwa ndiyo inayowasafirishia silaha hizo.

Katika wakati wake wa uongozi, Saleh amekusanya hifadhi kubwa ya silaha ikiwa ni pamoja na makombora, na yale yaliyorushwa katika ardhi ya Saudi Arabia hivi karibuni yanaweza kuwa yametengenezwa nchini Yemen, kama wanavyodai Wahouthi, licha ya kupingwa na Marekani pamoja na Saudia Arabia.

Wakati vita vilipoanza kulikuwa na usafiri wa anga wa moja kwa moja kati ya Iran na Yemen kwa upande wa Wahouthi, usafiri huo hauwezekani tena, jambo linalofanya vigumu kwa Iran kuwasaidia waasi hao. Hata hivyo, vidau bado vinatumika kusafirisha vifaa vidogo vidogo kupitia njia za pwani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape
Mhariri: Mohammed Khelef