1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yapunguza makali kwa Yemen

14 Novemba 2017

Uamuzi wa Saudi Arabia wa kupunguza vikwazo vyake vikali dhidi ya Yemen wiki moja tu baada ya kuviweka, inaonyesha nchi hiyo imesalimu amri kutokana na hatua yake hiyo kulaumiwa na kupingwa kimataifa. 

https://p.dw.com/p/2naM7
Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman
Picha: Reuters/Saudi Press Agency

Vilevile huenda Saudi Arabia ikawa inahofia kuonekana mbaya na katili kutokana na picha zinazosambaa mitandaoni zikiwaonyesha watoto wa Yemen pamoja na watu wazima walio dhoofika. Saudi Arabia sasa inajaribu kulegeza udhibiti wake katika nchi za Lebanon na Yemen. Jana Jumatatu, nchi hiyo ilitangaza kuwa kikosi cha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika kupambana na waasi wa Kishia  huko nchini Yemen vitaanza kufungua viwanja vya ndege na bandari katika nchi hiyo, siku kadhaa baada ya kuzifunga sehemu hizo kufuatia mashambulizi ya kombora la masafa marefu lililo ulenga mji mku wa Saudi Arabia, Riyadh.

Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa Abdallah Al Moualimi ndiye aliyetangaza hatua ya kufungua njia hizo. "Tungependa kuhahakisha kuwa hatua zinazochukuliwa na umoja tunao uongoza ni hatua tulizojadili na kukubaliana na serikali ya Yemen," amesema Al Moualimi. "Hatua hizi ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa mashirika yanayohusika na masuala ya kibinadamu na pia hii ni fursa kwa shughuli za usafiri wa vyombo vya usafiri wa binadamu na mizigo. Hatua ya kwanza ni kufunguliwa kwa viwanja vya ndege na bandari katika saa 24 kwenye maeneo yaliyo chini ya serikali ya Yemen."

Trump aunga mkono viongozi wa Saudi Arabia

Balozi huyo wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa amesema bandari zitakazofunguliwa ni ya Aden, Al Mukalla Mocha na pia na viwanja wa ndege vya Aden, Sayun na Socotra. Moualimi amemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa apeleke watalaamu kwenye makao yao makuu yaliyopo mjini Riyadh ili kwenda kukagua na kuhakikisha kuwa hatua zote zilizotajwa zinazingatiwa. 

Yezidi Sayigh Mwanazuoni mwandamizi wa chuo cha Carnegie cha masuala ya Mashariki ya Kati cha Beirut nchini Lebanon amesema matukio hayo yanaonyesha kuwa mwana mfalme wa Saudi Arabia anayependa kutumia vitisho na ubabe amebadili msimamo wake na kujaribu kuupoza mvutano wa Mashariki ya Kati lakini, akiongeza kuwa  kwa kiwango kikubwa  hayo yametokana na shinikizo la kimataifa.

Mohamed bin Salman mwana mfalme mwenye umri wa miaka 32 asiye na uzoefu katika masuala ya uongozi amepanda madaraka kwa haraka  katika kipindi cha miaka mitatu tu na katika muda huo mfupi masuala nyeti kama vile siasa, usalama na uchumi yamekuwa mikononi mwake. Akiwa  waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia yeye ndiye mwenye jukumu la vita vinavyoongozwa na nchi hiyo ya kifalme nchini Yemen. Salman anaungwa mkono na rais wa Marekani Donald Trump pamoja na mkwewe Jared Kushner ambaye ndiye mshauri wake mkuu  wa  masuala ya Mashariki ya kati.

Mwandishi: Zainab Aziz

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman