1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yapania kuizima Bayern Munich isitwae ubingwa.

23 Aprili 2010

Kombe la klabu bingwa na TP Mazembe

https://p.dw.com/p/N4jE
Schalke 04 kuizima Munich ?Picha: AP

KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA:

Duru ya tatu ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika inarudi uwanjani jioni hii, huku SuperSport Utd ya afrika kusini ikipambana na Heartland ya Nigeria.

Katika Kombe la Shirikisho -Confederations Cup,Simba ya Tanzania inapanga kunguruma mjini Dar-es-salaam kesho mbele ya Harras al Hodoud ya Misri.

Schalke imefunga safari ya Berlin leo ikiwa na azma moja tu: Kuizuwia Bayern Munich inayoongoza Ligi kwa pointi 2 kutawazwa mabingwa mapema.

Na zikisalia siku si zaidi ya 50 kabla ya firimbi kulia kwa kombe la dunia, Bafana Bafana iliokuwa Ujerumani wiki hii haikumudu zaidi ya sare na korea ya Kaskazini.

Mabingwa wa Kombe la klabu bingwa, TP mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, itakuwa uwanjani kesho Jumapili mjini Bamako, Mali, kutetea taji lao bila ya uzembe uwanjani mwa Djoliba wakati mjini Tripoli, Libya, Al-Ittihad itattembelewa na majirani zao Al Ahly kutoka Misri, mabingwa mara 6 wa kombe hili. Huko Omdurman, Sudan, Al Hilal ina miadi pia kesho na majirani zao wengine Ismailia ya Misri ,wakati huko Tizi-Ouzou, Algeria, JS Kabylie wanapambana na Petro Atletico ya Angola. Kalenda ya kesho itakamilishwa kwa zahama mjini Harare baina ya Dynamos na Gabarone United ya Botswana.

Jioni ya leo, lakini, uwanjani mjini Johannesberg, ni wenyeji SuperSport Utd. ya Afrika Kusini, ikichuana na Heartland ya Nigeria. Huko Setif, Algeria , Entiente Setif inawakaribisha nyumbani Zanaco kutoka Zambia. Duru ya mwishoni mwa wiki hii ya Kombe hili la Afrika, ilifunguliwa jana Ijumaa kwa changamoto kati ya Esperence ya Tunisia na Al-Merreikh ya Sudan.

Ama katika kinyan'ganyiro cha Kombe la Shirikisho, madume wa Tanzania, Simba, walionguruma nyumbani kwa kutwaa taji la ubingwa , wameahidi kunguruma tena kesho Mzizima (Dar-es-salaam) na kuwaonesha wageni wao kutoka Uarabuni, nani ni sultani wa dimba mjini humo. Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, itaikaribisha Kinshasa Enyimba ya Nigeria. Warri Wolves-mbwa mwitu wa Nigeria, wamepanga kuwatafuna CAPS United kutoka Zimbabwe.

"Mla ,lakini, ni mla leo, mla kesho kala nini ?

Cotonsport-Garoua ya Kameroun , imeiahidi Primerio Agosto ya Angola, kuionesha "kilichomtoa kanga manyoya". Na mjini Niamey, Niger, AS Fan inacheza na Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

BUNDESLIGA NA PREMIER LEAGUE:

Kinyan'ganyiro cha ubingwa kimepamba moto tangu katika Premier League-Ligi ya Uingereza ambako viongozi Chelsea, waliteleza mwishoni mwa wiki iliopita na kuwapa moyo tena Manu ya kuvaa taji; na katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani ambamo Bayern Munich inatamba wakati huu ikiwa na kiu ya vikombe 3:

Inavyoonesha sasa, ni Schalke tu iliopo pointi 2 nyuma ya Munich, inayoweza kuitia munda Bayern Munich isiondoke na taji la Bundesliga. Kocha wao, Felix Magath, alieitawaza Wolfsburg msimu uliopita mabingwa wa Ujerumani , ana shabaha hiyo.

Schalke, ina miadi leo na Hertha Berlin. Berlin inahitaji alao pointi 5 katika mapambano 3 yaliosalia kumaliza msimu ili iokoe isizame daraja ya pili. Kwa hivyo, Schalke ina kibarua kigumu jioni hii huko Berlin, kurudi nyumbani na pointi 3 ambazo lazima iondoke nazo ili kuweka hayi matumaini yake ya ubingwa.

Bayern Munich, baada ya kuzima vishindo vya Olympique Lyon juzi, katika Champions League na sasa ina matumaini ya kucheza finali ya Kombe hilo, pia ina changamoto kali nyumbani mwa Borussia Moenchengladbach jioni hii.

Leverkusen, iliopo nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi, ina hamu ya kuingan'gania nafasi hiyo ispokonywe na Werder Bremen inayokuja juu kwa kasi. Leverkusen leo iko nyumbani ikicheza na Hannover. Borussia Dortmund , imeitembelea Nuremberg, wakati Bremen, ni wenyeji wa FC Cologne. Mainz inacheza na Frankfurt.

Kesho, Jumapili, duru hii ya Bundesliga itakamilishwa kwa changamoto mbili: Hoffenheim itacheza na Hamburg, iliofaulu kutoka suluhu tu 0:0 juzi na Fullham katika Kombe la Ligi la Ulaya. Freiburg itaikaribisha mabingwa Wolfsburg.

Katika changamoto za Premier League , mwishoni mwa wiki hii, Manchester United iko uwanjani Old Traford ikicheza na Tottenham Hotspur, wakati Chelsea, wana miadi kesho na Stoke City. Bolton Wanderers, wanaiwaga Portsmouth, itayorudi daraja ya pili msimu ujao. West Ham United inapambana na Wigan Athletics. Liverpool, iliolazwa bao 1:0 katika Kombe la Ulaya wiki hii, itaitembelea Burnley kesho.Everton inacheza na Fulham ambayo imemudu sare na Hamburg ya Ujerumani , katika Kombe la Ulaya kati ya wiki hii.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE/AFPE/DPAE

Uhariri: Miraji Othman