1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Coe ajiuzulu kama balozi wa NIKE

27 Novemba 2015

Rais wa IAAF Sebastian Coe ameapa kurejesha imani katika shirikisho hilo la riadha la kimataifa baada ya msururu wa kashfa za rushwa na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu ambazo zimeuchafua riadha

https://p.dw.com/p/1HDeq
Weltverband IAAF-Präsident Sebastian Coe
Picha: Getty Images/L. Zhang

Akizungumza baada ya mkutano wa Baraza la IAAF, Coe alijiuzulu wadhifa wake kama balozi wa NIKE kuhusiana na kile baadhi ya watu walielezea kuwa ni mgongano wa maslahi, hasa kuhusiana na kupewa kibali mji wa Eugine kuandaa mashindano ya dunia ya mwaka wa 2021, mji ambao uko katika jimbo la Oregon ambako ndiko kunapatikana kampuni hiyo kubwa ya bidhaa za michezo.

Coe amesema "Safari ya kurejesha imani siyo ya kisanyansi. Hakuna uhakika katika hili lakini inastahili kuanza kwa kuhakikisha kuwa tuna shirikisho ambalo liko tayari kutekeleza majukumu na kutoa huduma linalostahili kutoa na linaweza kuendeleza na kujenga hadhi ambayo imeathirika vibaya kabisa katika wiki chache zilizopita. Muda ambalo hilo litafanyika sijui. Kwa jumla huenda likafanyika hata baada ya muhula wangu".

Coe amesema kuwa mchakato wa kuleta mabadiliko katika IAAF na riadha ambao ndio mchezo muhimu katika Mashindano ya Olimpiki, utachukua muda.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Josephat Charo