1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Coe ampiku Bubka katika uchaguzi wa IAAF

19 Agosti 2015

Bodi ya Shirikisho la Kimataifa la riadha IAAF, imemchagua Sebastian Coe kuwa rais wake mpya, katika uchaguzi uliofanywa mjini Beijing, China

https://p.dw.com/p/1GHfr
China IAAF Sebastian Coe schüttelt Sergej Bubka die Hand
Picha: Getty Images/IAAF/A. Hassenstein/

Coe amembwaga mpinzani wake Sergei Bubka kutoka Ukraine kwa kupata kura 115 dhidi ya 92 za Bubka na atachukua usukani kutoka kwa rais wa IAAF Lamine Diack mwenye umri wa miaka 82. Raia huyo wa Senegal anajiuzulu baada ya kuongoza kwa miaka 16.

Katika mkutano na waandishi habari, Coe hakuweka bayana juu ya suala la kitengo maalumu kitakachoanzishwa ili kupambana na tatizo la matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Lakini ametetea uadilifu wa bodi iliyoko madarakani na kuahidi utendaji uliotukuka katika kuiimarisha sera ya kutokuvumilia kuhusu dawa za kulevya.

Coe mwenye umri wa miaka 58, alishinda dhahabu ya mbio za mita 1,500 katika Michezo ya Olimpiki ya 1980 na 1984 na akaishikilia rekodi ya ulimwengu katika mita 800 kwa miaka 16. Alikuwa kiongozi wa kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya London 2012 na Makamu wa Rais wa IAAF na anapigiwa upatu kuchukua wadhifa wa rais.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba