1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sekta ya mafuta Uganda kwenye kashfa nzito

23 Mei 2013

Hata kabla ya uchimbaji wa mafuta kuanza, sekta ya mafuta nchini Uganda imekumbwa na madai ya hongo dhidi ya maafisa wa serikali, kesi zinazohusiana na kodi nje ya nchi, ambazo zinaigharimu serikali mamilioni ya pesa.

https://p.dw.com/p/18buK
Ugandan President, Yoweri Museveni speaks during the London Summit on Family Planning organized by the UK Government and the Bill & Melinda Gates Foundation with the United Nations Population Fund, UNFPA, in central London Wednesday July 11, 2012. (Foto:Carl Court, Pool/AP/dapd)
Präsident von Uganda Yoweri MuseveniPicha: dapd

Uganda ambayo imethbitisha kuwa na hifadhi ya kiasi cha pipa bilioni 3.5 inataka kuchimba angalau kiasi cha pipa bilioni 1.2 katika kipindi cha miongo mitatu ijayo. Idadi hiyo inaweza kuongezeka pale maeneo mengine yatakaponza kufanyiwa utafiti baadae mwaka huu, na hivyo kuifanya nchi kuwa moja ya mataifa kunakochimbwa mafuta kwa wingi barani Afrika.

Lakini baadhi ya wataalamu na wachambuzi wana wasiwasi kuwa nchi hiyo imekuwa na mwanzo mbaya, na inaendelea kuwa na ukosefu mkubwa wa utulivu wa kisiasa, ambao ungeisaidia kuepuka baadhi ya makosa yaliyofanywa na mataifa mengine yaliyo na utajiri wa mafuta lakini yenye viwango vikubwa vya umaskini.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amejipa haki ya kuwa na kauli ya mwisho kabla ya kusainiwa kwa makubaliano yoyote na makampuni ya mafuta, akisema kuwa sera hiyo inalenga kuhakikisha kuwa maslahi ya nchi yanaendelea kulindwa.

Museveni akosolewa

Lakini wakosoaji wanasema ushiriki wa karibu wa rais hauna msaada kwa nchi ambayo inahitaji kujikita katika ujenzi wa taasisi zinazoaminika na zilizo na uwazi ili ziweze kusimamia utajiri unaotokana na mafuta hayo hata kama Museveni yupo au la.

Harakati za mafuta nchini Uganda.
Harakati za mafuta nchini Uganda.Picha: picture alliance/dpa

Katika kikao cha bunge kilichosababisha kelele kutoka kwa umma, mbunge wa kujitegemea aliwanyooshea kidole mawaziri watatu ambao aliamini walihongwa na kampuni za mafuta za kigeni zilizokuwa zinataka kuingia mikataba na serikali ya Uganda.

Tuhuma hizo ambazo zilikanushwa na mawaziri hao watatu ziliwalaazimu wabunge wa kambi zote kuagiza uchunguzi ambao wengi walitumai ungekuwa wa haraka na usio na mashaka. Karibu miaka miwili baadae, uchunguzi huo bado unaendelea na Gerald Karuhanga, mbunge alietoa tuhuma hizo kwa mara ya kwanza, anasema hatazamii kuona ripoti ikitolewa.

Uganda haijawahi kuwa makabidhiano ya amani ya madaraka tangu ilipopata uhuru mwaka 1962, na museveni mwenyewe, akiwa madarakani tangu mwaka 1986, anazidi kukabiliwa na shinikizo la kustaafu.

Utoaji mafuta kuanza 2016

Uganda, ambayo ilitangaza kuwa na viwango vikubwa vya mafuta mwaka 2006, inatarajia kuwa mtoaji wa mafuta ghafi kufikia mwaka 2016. Huo ndiyo muda ambapo muhula wa sasa wa Museveni utakuwa unakaribia kuisha, na wengi wanaamini atagombea tena.

Mfanyakazi wa uchimbaji mafuta wa Kichina nchini Uganda.
Mfanyakazi wa uchimbaji mafuta wa Kichina nchini Uganda.Picha: Getty Images

Kuingilia kwa Museveni katika masuala ya mafuta kunaifanya Uganda isivutie kwa wawekezaji wa kigeni, kwa mujibu wa shirika la ushauri wa hatari za kisiasa (Eurasia), lenye makao yake mjini New York Marekani.

Shirika hilo limesema katika ripoti yake iliyotolewa mwezi uliyopita, kuwa kuongezeka kwa kutoelewana ndani ya chama tawala nchini humo NRM, ambapo wanachama vijana wanashinikiza kuwepo na uongozi mpya, kumesababisha kuongezeka micutano.

Sheria mpya inampa waziri wa nishati, ambae ni mteule wa rais, mamlaka ya kutoa na kunyanganya mkataba. Baadhi wanasema kuwa ingawa hili linaweza kupunguza rushwa miongoni mwa maafisa wa serikali, lakini ushiriki wa karibu wa rais unadhoofisha uendelezaji wa taasisi kama vile kampuni ya taifa ya mafuta ambayo inapangwa kuanzishwa.

Makubaliano ya kampuni za kigeni

Uganda na kampuni tatu za kigeni walifikia makubaliano mwezi uliyopita, ambayo yanahusisha ujenzi wa bomba litakalosafirisha mafuta ghafi kupitia Kenya. Kampuni ya Total kutoka Ufaransa na CNOOC ya China, ambazo zilinunua theluthi mbili ya mali za kampuni ya Tullow kutoka Uingereza kwa dola bilioni 2.9 mwaka uliyopita, zitajenga mtambo wenye uwezo wa kusafisha pipa 30,000 kwa siku.

Lakini makubaliano ya mwisho bado hayajafikiwa, kwa sehemu kutokana na kile ofisi ya rais ilichosema ni kutokubaliana, kuhusu namna ya kuendeleza bomba la kusafirisha na mtambo wa kusafisha.

Makadirio ya sasa ya utajiri wa mafuta ya Uganda yako katika asilimia karibu 40 ya utafiti uliyofanywa katika eneo lililo karibu na ziwa Albert, mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Katika wiki zijazo maafisa wa serikali wanatarajiwa kuzialika kampuni kuomba zabuni kwa ajili ya kupatiwa leseni za utafiti katika viwanja visivyopungua 13, katika mchakato ambao wanaharakati wanatumai utakuwa wa uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa mara iliyopita.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman