1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal: Vyama vya upinzani vyaunda muungano

12 Machi 2012

Kampeni za duru ya pili ya uchaguzi wa Rais zimeanza nchini Senegal. Vyama vya upinzani vimejiunga pamoja katika juhudi za kumzuia Rais Abdulaye Wade kuchaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha tatu.

https://p.dw.com/p/14JES
Karatasi za kupigia kura Senegal
Karatasi za kupigia kura SenegalPicha: Reuters

Maelfu ya Wasenegal jana walihudhuria mandamano yaliyoitishwa na wagombea 12 wa uchaguzi wa Rais ambao katika duru ya kwanza ya uchaguzi walishindwa kupata kura za kutosha. Wagombea hao wamejiunga pamoja kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani wa Senegal, Macky Sall, ambaye ndiye mpinzani mkuu wa Abdulaye Wade.

Maandamano hayo yalifanyika katika uwanja wa Obelisk, mahali ambapo tayari maandamano ya kuupinga uamuzi wa Wade kugombea tena yalifanyika katika kipindi cha takriban mwezi mmoja. Maandamano hayo yaliyoambatana na vurugu yalisababisha vifo vya watu sita na watu wapatao 150 kujeruhiwa.

Macky Sall apewa nafasi kubwa ya kushinda

Jumamosi iliyopita, Macky Sall alitangaza kuundwa muungano wa vyama vya upinzani unaojiita Alliance of Forces for Change. Muungano huo unaundwa na vyama vyote vya upinzani ambavyo havikupata kura za kutosha kwa ajili ya kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi, Wade alipata asilimia 34.8 ya kura, huku Sall akipata asilimia 26.5. Lakini kura za muungano wa vyama vya upinzani zikijumlishwa, zinafikia asilimia 60. Hivyo Sall anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi utakaofanyika tarehe 25 mwezi huu.

Mgombea wa urais Macky Sall
Mgombea wa urais Macky SallPicha: AP

Abdulaye Wade, mwenye umri wa miaka 85, amekuwa madarakani kwa miaka 12 sasa. Rais huyo anashutumiwa kuibadilisha katiba ili apate haki ya kugombania urais katika awamu ya tatu.

Wade azishutumu nchi za Magharibi kufanya kampeni dhidi yake

Katika uchaguzi wa duru ya pili, Wade anategemea sana kupata kura za jumuiya za kiislamu. Lakini baadhi ya watu waliomuunga mkono hapo awali sasa wamehamia upande wa upinzani. Mmoja wao ni Waziri Mkuu wa zamani wa Senegal, Moustapha Niasse.

Rais Abdulaye Wade aliyeko madarakani
Rais Abdulaye Wade aliyeko madarakaniPicha: AP

Wade ameliambia shirika la habari la Senegal kwamba alishindwa kupata kura za kutosha katika duru ya kwanza kwa sababu ya kile alichokieleza kuwa kampeni za nchi za Magharibi dhidi yake. Marekani na Ufaransa zimemshauri Rais huyo aachie madaraka. Ingawa Wade anatambulika kama Rais aliyefanya juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu nchini mwake, wahakiki wanasema kwamba mara nyingi Wade ameipa kupaumbele miradi mikubwa badala ya kujali kwanza masuala ya uongozi bora.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE

Mhariri: Othman Miraji