1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yasitisha kumrudisha Habre nchini Chad

11 Julai 2011

Senegal imesitisha kwa muda uamuzi wa kumrudisha nyumbani aliyekuwa Rais wa Chad, Hissene Habre, kukabiliana na adhabu ya kifo, baada ya uingiliaji kati wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/11sra
Rais Abdulaye Wade wa Senegal
Rais Abdulaye Wade wa SenegalPicha: picture-alliance/dpa

Uamuzi huu mpya unatokana na ombi la Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ambaye katika taarifa yake ya mapema hapo jana (10 Julai 2011) aliitaka serikali ya Senegal ipitie upya uamuzi wake wa kumrudisha Habre nchini Chad, vyenginevyo iwe na uhakika kuwa kiongozi huyo wa zamani atapatiwa hukumu ya haki na hatokabiliana na mateso au kunyongwa.

Katika tamko lake kupitia televisheni ya taifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal, Madicke Niang, jioni ya jana alibatilisha uamuzi huu kwa muda.

"Kufuatia ombi la Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu, Senegal inasitisha hati ya kumrudisha Habre." Amesema Niang.

Senegal, ambayo imesaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Mateso, haiwezi kumsafirisha mtu kumpeleka kwenye nchi ambayo ina ushahidi wa kutosha wa kuamini kuwa atateswa.

Habre (69) aliondolewa madarakani kwa mapinduzi mwezi Disemba mwaka 1990 na rais wa sasa, Idris Deby. Anatuhumiwa kwa mauaji ya maelfu ya watu na mateso mengine yaliyofanyika katika kipindi cha utawala wake wa miaka nane kwenye taifa hilo la Afrika ya Kati.

Habre ameishi nchini Senegal tangu kupinduliwa kwake, licha ya jitihada za kutaka kumshitaki aidha ndani ya Senegal au kwenye nchi nyengine.

Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre
Rais wa zamani wa Chad, Hissene HabrePicha: dpa

Mwanasheria wa Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch, Reed Brody, ambaye amekuwa akifuatilia kesi ya Habre kwa miaka mingi, amesema kwamba Shirika lake limefurahishwa na uamuzi huu wa serikali ya Senegal, ingawa hicho kisichukuliwe kuwa kigezo cha Habre kuepuka mkono wa sheria.

"Baada ya miaka 20, wahanga wake wana haki ya kupata haki yao kupitia mahakamani. Kupelekwa kwa Habre nchini Ubelgiji hivi sasa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa anajibu mashitaka dhidi yake pakiwa na uhakika mkubwa wa kupatiwa hukumu ya haki." Amesema Brody.

Hapo mwaka 2005, jaji mmoja nchini Ubelgiji alitoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa rais huyo wa zamani kufuatia kesi iliyofunguliwa dhidi yake. Tangu wakati huo, Ubelgiji imekuwa ikipigania kuwa Habre abakie Senegal hadi kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa itakapomalizika na pia asirudishwe nchini Chad.

Kabla ya taarifa ya serikali ya Senegal ya jioni ya jana kusitisha uamuzi wa kumrudisha Habre nchini Chad, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji ilisema inasikitishwa na namna Senegal inavyodharau wajibu wake kwa Mahakama ya Kimataifa ya The Hague.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka 10, palikuwa na mgogoro kati ya Senegal na mashirika ya haki za binaadamu juu ya kushitakiwa kwa Habre, ambapo mwanzoni Senegal ilisema haikuwa na sheria ya kumshitaki, lakini hata sheria ilipotungwa, ikasema haikuwa na pesa za kuendeshea kesi.

Habre na viongozi wengine 11 wa makundi ya waasi wa mashariki, walihukumiwa kifo hapo mwezi Agosti mwaka 2008 nchini Chad bila ya yeye kuwapo mahakamani.

Hukumu hiyo ilitokana na kuvamiwa na kuzingirwa kwa ikulu ya Rais Deby mjini N'Djamena na waasi, kabla ya waasi hao kufukuzwa na majeshi ya Rais Deby. Habre na wenzake hao walitiwa hatiani kwa kuhatarisha usalama na katiba ya nchi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Thelma Mwadzaya