1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SEOUL: Korea Kusini yalaani mauaji ya raia wake Afghanistan

26 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBf5

Korea Kusini imelaani vikali kuuwawa kwa raia wake mmoja aliyekuwa miongoni mwa mateka 23 wa nchi hiyo wanaozuiliwa na wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan.

Wanamgambo wa Taliban walimpiga risasi na kumuua mateka huyo jana baada ya kuonya wangeanza kuwaua baadhi ya mateka ikiwa serikali ya Afghanistan haingewaachilia huru wafungwa wa Taliban walio gerezani.

Katika taarifa iliyotangazwa kwenye runinga ya taifa mpambe wa rais wa Korea Kusini amesema kuwaumiza raia wasio na hatia hakuwezi kuhalalishwa.

Wakorea kusini 23 wakiwemo wanawake 18 na wanaume watano waliokuwa wakifanyakazi ya kujitolea kwenye mradi ulioandaliwa na kanisa moja la mjini Seoul, walitekwa nyara katika barabara kuu kutoka kusini mwa Kabul Ijumaa iliyopita.

Wakati huo huo, maiti ya mhandisi mjerumani aliyetekwa nyara Jumapili iliyopita imewasili hapa Ujerumani. Mjerumani wa pili angali anazuiliwa na wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Taliban.