1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera madhubuti njia sahihi kuondokana na umaskini

5 Desemba 2013

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati kutoka Jumuiya za kiraia wamesema sera madhubuti kuzungumzia umaskini, njaa na uharibifu wa mazingira ni njia pekee ya kuondokana na baa la njaa na umaskini.

https://p.dw.com/p/1ATmS
Watu bilioni moja wanaishi katika umaskini wa kupindukia duniani.
Watu bilioni moja wanaishi katika umaskini wa kupindukia duniani.Picha: AP

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametaja kuwa zaidi ya watu bilioni moja bado wanaishi katika umaskini wa kupindukia na zaidi ya watu milioni 840 wanakabiliwa na njaa.

Danielle Nierenberg, mmoja wa waanzilishi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linaloshughulikia masuala ya chakula lenye makao yake nchini Marekani, amesema inapaswa kutafuta njia za haraka za kuondokana na baa la njaa na umaskini, duniani.

Wakati wa mkutano kupanga mpango wa maendeleo endelevu ya milenia utakaozinduduliwa rasmi mwakani, maafisa hao wamesema kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kukabiliana na mzizi unaosababisha umaskini na ukosefu wa chakula na njia sahihi za kuzuia uharibifu wa mazingira.

Hivyo basi serikali, wafanyabishara, wakulima na mashirika ya kiraia, watambue kwamba wakati wa kuchukua hatua ni sasa, hususan katika kipindi hiki ambapo mabadiliko ya tabia nchi yanachukua nafasi katika dunia nzima, anasema Nierenberg ambaye pia ni mkurugenzi wa zamani wa mpango wa chakula na kilimo, mjini Washington.

2030 kikomo cha umaskini na njaa?

Mkutano wa viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa chini ya uenyekiti wa wakuu wa nchi kutoka Indonesia, Liberia na Uingereza mwaka jana ulitoa mwongozo uliolenga kuondoa umaskini na njaa hadi ifikapo mwaka 2030, lakini ni namna gani lengo hilo litafanikiwa iliachwa mikononi mwa kamati maalum iliyoundwa ikijumusha nchi 30 mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ambayo inatarajia kuwasilisha mapendekezo yake mwakani.

Mpango wa maendeleo ya milenia; unalenga kupunguza hadi kufikia nusu ya idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa kupindukia na baa la njaa ifikapo mwaka 2015, ingawa lengo hilo linaweza lisifikiwe na mataifa mengi maskini, hasa kutoka Bara la Afrika.

Ukame ni moja ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Ukame ni moja ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.Picha: ABDELHAK SENNA/AFP/GettyImages

Ingawa kwa mujibu wa mkurugenzi msaidizi wa Shirika la Kilimo na Chakula, Jomo Kwame Sundaram, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa shirika hilo bado linajitolea kusimamia lengo lake kuhusu usalama wa chakula na lishe, ikiwa ni pamoja na kuondoa umaskini na utapiamlo na kwamba ni vigumu kubainisha ni kwa vipi malengo ya maendeleo ya milenia yamechangia kupunguza idadi ya watu wanaoishi kwenye umaskini.

Wasi wasi kufikiwa lengo la milenia

Kufuatia kuundwa kwa kamati ya ngazi za juu kuangalia usalama wa chakula duniani na ikizingatiwa kupanda kwa bei ya vyakula mapema mwaka 2008, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alionyesha wasi wasi wake kuhusu kufikiwa kwa lengo hilo la milenia la kuondokana na njaa.

Mwaka jana katibu mkuu huyo alimteua mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula, Jose Graziano da Silva alipozindua kampeni ya kutokomeza baa la njaa, wakati wa mkutano wa 20 mwaka jana kuhusu masuala ya chakula.

Maafia hao wamesema kuwa mapambano dhidi ya ukosefu na uharibifu wa chakula ni mfano mzuri wa namna wakulima, wafanyabiashara na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanavyoweza kufanya kazi kwa pamoja kutengeneza miundo mbinu iliyo bora, kulinda mazao, na kuwa na njia bora za upatikanaji wa chakuala ambacho kingeweza kuharibiwa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon.Picha: picture alliance/abaca

Wamesema kuna umuhimu mkubwa kuzingatia suala la kilimo na njia mbadala za kutatua matatizo kama vile changamoto za kimazingira na kijamii ikiwa ni katika ukosefu wa ajira, migogoro,ongezeko la watu mijini na hata mabadiliko ya tabia nchi, wakati wa mikutano kutathimini malengo ya maendeleo ya milenia mwakani.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman