1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera za Misaada ya Maendeleo ya Ujerumani

M.Fürstenau - (P.Martin)3 Septemba 2008

Mkutano wa kimataifa unaojadili manufaa ya ushirikiano katika miradi ya maendeleo umefunguliwa mji mkuu wa Ghana Accra.

https://p.dw.com/p/FAnQ
Bundesentwicklungshilfeministerin Heidemarie Wieczorek-Zeul (SPD) stellt am Montag (03.09.2007) in Berlin den neuen entwicklungspolitischen Freiwilligendienst "weltwärts" vor. Ab 2008 können junge Menschen zwischen 18 und 28 Jahren einen Freiwilligendienst in Afrika, Lateinamerika, Asien oder Osteuropa absolvieren. Foto: Peer Grimm dpa/lbn +++(c) dpa - Report+++
Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani,Heidemarie Wiezcorek-Zeul.Picha: picture-alliance/dpa

Kutoka Ujerumani miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Misaada ya Maendeleo,Heiedemarie Wieczorek-Zeul wa chama cha SPD.

Tuhuma za tangu zamani zingali zikiendelea:yaani kutoka mabilioni yaliyotolewa na nchi wafadhili ni pesa chache tu zilizofika kwa masikini. Madai hayo yaliibuka upya siku ya Jumatatu.Kwa mujibu wa wataalamu wa kisiasa na vyombo vya habari,mageuzi makubwa yanahitaji kufanywa.

Kwani kiasi ya asilimia 80 ya misaada inayotolewa hutumiwa kwa urasimu na serikali zinazopokea misaada,ambazo mara nyingi zinahusika na ufisadi. Wataalamu wanaotaka mageuzi katika sera za misaada ya maendeleo wanasema,kinachopaswa kufanywa ni kushughulikia zaidi miradi ya mikopo midogo,elimu na miundombinu.

Lakini kwa maoni ya Waziri Heidemarie Wieczorek-Zeul mambo yanayodaiwa na wakosoaji,tangu hapo ni sehemu ya ajenda ya kisiasa.Si hayo tu ,bali uwazi pia ni jambo linalohitajiwa kutoka pande zote mbili.Anaongezea:

"Nchi shirika zinapaswa kueleza waziwazi msaada huo unapelekwa wapi na unatumiwa vipi.Huo ni wajibu wa nchi zinazoendelea.Lakini sisi vile vile tunapaswa kutoa maelezo ya hesabu na habari zinazohusika na miradi ya misaada."

Lakini hilo ndio linalokosekana anasema Karl Addicks,mwanasiasa wa chama cha kiliberali cha Ujerumani FDP.Mradi wa kugharimia sehemu ya bajeti katika baadhi ya nchi zinazoendelea,ambao huungwa mkono na waziri wa maendeleo wa Ujerumani,unakaribishwa,lakini kwa masharti maalum.Na masharti hayo kwa mfano hayatimizwi na Msumbiji,nchi iliyotembelewa na Addicks hivi karibuni.Juu ya hivyo Msumbiji itapokea msaada zaidi wa fedha kutoka Ujerumani.Addicks anasema:

"Nchi kama hiyo isipatiwe msaada wa bajeti kwani serikali haizingatii haki za wapinzani.Hakuna uhuru wa vyombo vya habari na hiyo ni njia ya kuwa na udhibiti fulani."

Hata hivyo Karl Addicks anaetembelea sana nchi za Kiafrika,ameona mifano inayotia moyo na Rwanda ni miongoni mwa nchi hizo.Anasema,mtu hujionea moja kwa moja kuwa nchi hiyo inajitahidi:kwa hivyo hata waliberali wapo tayari kabisa kutoa msadaa zaidi kugharimia bajeti yake.Lakini kusaidia bajeti za nchi zenye ufisadi si jambo linaloungwa mkono na FDP.

Kimsingi,misimamo ya chama tawala cha SPD na FDP cha upinzani nchini Ujerumani haitofautiani hivyo.Kwani hata waziri wa maendeleo anasema, kinachohitajiwa ni kuimarisha haki za bunge na jamii za kiraia na kupiga vita rushwa.Vile vile nchi zinazopokea na zinazotoa misaada zinahitaji kuwa na uratibu ulio bora zaidi.