1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serekali mpya ya Wapalastina inaapishwa leo.

16 Machi 2007

Jana kutwa Wapalastina walilisheherekea lile tangazo lililongojewa kwa muda mrefu la wao kuwa na serekali ya Umoja wa Taifa baada ya kujionea miezi 12 ya mivutano mikali ya umwagaji damu katika kuwania madaraka, kutengwa kimataifa na kuwa na ugumu wa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/CHHz
Waziri mkuu-mteule, Ismail Haniya, na rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas.
Waziri mkuu-mteule, Ismail Haniya, na rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas.Picha: AP

Waziri mkuu mteule na kiongozi wa Hamas, Ismail Haniya, ataiwasilisha serekali yake mpya pamoja na programu yake ya kisiasa mbele ya bunge hii leo.

Akitangaza kuundwa serekali hiyo mpya, waziri mkuu-mteule, Ismail Haniya, alisema:

+Nina risala kwa Wapalastina walioko nchini na walio ngambo. Leo usiku, baada ya kuyatanzua matatizo yote, tumeunda serekali ya Umoaj wa Taifa na tumelitanzua suala la nani awe waziri wa mambo ya ndani.+

Wabunge wanatarajiwa karibu wote kwa kauli moja kuipa kura ya imani serekali mpya ya mseto ambayo itakiunganisha chama cha Hamas, chenye siasa kali za Kiislamu, na Chama cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas. Baada ya leo serekali hiyo kupigiwa kura, mawaziri watakula kiapo katika mji wa Gaza ifikapo jioni. Wale mawaziri wanaotokea Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambao hawataweza kwenda Gaza kutokana na vizuizi walivowekwa na serekali ya Israel wataapishwa siku ya pili huko huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Chama cha Hamas kitachukuwa nafasi 12 katika baraza la mawaziri lijalo kati ya 25, huku Chama cha Fatah cha Rais Abbas kitakuwa na mawaziri sita. Wizara saba, zikiwemo zile muhimu za fedha, mambo ya kigeni na mambo ya ndani, zitakwenda kwa watu wenye kujitegemea wenyewe, wasiokuwa na vyama, pamoja na wale wa kutoka makundi madogo.

Wapalastina wanataraji kwamba serekali mpya itafungua enzi ya utulivu na neema ya kiuchumi baada ya kujionea mwaka mzima wa umwagaji damu na serekali yao kususiwa.

Gazeti la kila siku la al-Quds liliandika leo kwamba Wapalastina, viongozi wao wote, makundi na vyama wameipita ile hatua ya mapigano ya kishenzi na wamepata mafanikio makubwa ya kitaifa, tena yalio muhimu na ya kihistoria.

Matarajio hayo yalitiliwa nguvu na picha ya katuni iliotoa sura ya serekali mpya ya Umoja wa Taifa ambayo inapita katika ufa wa ukuta wa mawe uliopewa jina la Ususiaji wa kimataifa.

Katika barabara nyembamba na katika kambi za wakimbizi walio maskini katika Ukanda wa Gaza, ambako malumbano baina ya vyama vya Hamas na Fatah yalikuwa makali kabisa, wakaazi waliezea matumaini. Mwanamke mmoja huko Khan Yunis, kusini mwa ukanda huo, Sana al-Masry, alisema wao wana furaha sana kwa kupatikana serekali ya Umoja wa Taifa, kwa sababu hawataki kuweko mapigano zaidi baina ya Hamas na Fatah. Alisema kilicho muhimu ni serekali mpya iikomeshe hali ya Palastina kuzingirwa, iunde nafasi za kazi, ifunguwe mipaka na iwalipe mishahara wafanya kazi wake. Mfugaji wa kuku, Zuhair Abdullah, alipumua na kusema wao wamechoka na matatizo na mateso walioyapata katika mwaka mzima, na kwamba wakati umefika wa kuboresha hali za watu.

Licha ya kufikiwa muwafaka huo wa kuundwa serekali ya Wapalastina, jamii ya kimataifa haijatoa ishara kubwa kwamba itaregeza vikwazo vya kifedha ilivoviweka dhidi ya serekali ya hapo kabla iliokuwa inaongozwa pekee na Chama cha Hamas.

Israel jana ilisema kwamba serekali hiyo ya Umoja wa Taifa ni hatua ya kurejea nyuma, na kwa haraka ikakataa kama kutakuweko kuregeza kamba. Marekani na Umoja wa Ulaya hazijatoa ahadi, zikisema hazitatoa hukumu juu ya serekali hiyo hadi pale watakapouchunguza mpango wa baraza hili jipya la mawaziri.

Makamo wa waziri wa ulinzi wa Israel, Ephraim Sneh, alisisitiza juu ya msimamo usiotetereka wa serekali ya nchi yake unaohimiza kuweko ushirikiano na Rais Abbas ili kukivunja nguvu chama cha Hamas.

Pande nne zinazohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati- yaani Umoja wa Ulaya, Russia, Umoja wa Mataifa an Marekani- ziliweka vikwazo vya kuipatia fedha serekali ya Wapalastina mwaka mmoja uliopita pale Chama cha Hamas, kinachoangaliwa na Israel kuwa ni kundi la kigaidi, kilipoingia madarakani. Pande hizo nne zimeshikilia kwamba serekali ya Wapalastina iachane na matumizi ya nguvu, iitambuwe Israel na ikubali kuambatana na mikataba ya hapo kabla. Yakitimizwa hayo hapo ndipo fedha zitarejea kummiinika huko Palastina.