1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali kukutana na waasi wa Darfur

P.Martin7 Septemba 2007

Serikali ya Sudan nawaasi kutoka jimbo la Darfur watakutana tarehe 27 Oktoba nchini Libya.

https://p.dw.com/p/CH8O
Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akizungumza na mjumbe wa UNICEF katika kambi ya wakimbizi ya Al-Salaam,kwenye jimbo la Darfur
Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akizungumza na mjumbe wa UNICEF katika kambi ya wakimbizi ya Al-Salaam,kwenye jimbo la DarfurPicha: AP

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-Moon na Rais wa Sudan, Omar al-Bashir mjini Khartoum.

Taarifa hiyo inatazamwa kuwa ni mafanikio ya ziara ya kwanza ya Ban Ki-Moon nchini Sudan,kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Baada ya kutembelea jimbo la mgogoro la Darfur,Ban ameukumbusha ulimwengu hali ya Darfur iliyoelezwa na mtangulizi wake kama ni maafa makubwa kabisa ya kiutu,wakati huu wa sasa.

Alipotembelea kambi ya wakimbizi ya Al Salaam katika jimbo la Darfur, Ban aliwaambia wakazi wa kambi hiyo,amekwenda huko kuwapelekea ujumbe wa matumaini.Yadhihirika kuwa ujumbe huo umetimika,kwani serikali na waasi wa Darfur wamekubali kukutana kwa majadiliano ya amani. Katibu Mkuu Ban amesema,hatua kubwa imechukuliwa kuelekea lengo la pamoja kwa azma ya kuleta amani katika Darfur na pia maendeleo ya muda mrefu kwa Sudan.

Hatua ya kwanza ilichukuliwa mwezi uliopita, makundi mbali mbali ya waasi yalipokutana Arusha,nchini Tanzania na kuafikiana kuwa na msimamo mmoja dhidi ya serikali.Hatua ya pili muhimu ni mkutano utakaofanywa nchini Libya. Katika mkutano huo,madai makuu ya waasi ni baadhi ya sababu zilizochochea mgogoro wa Darfur:yaani kinyanganyiro cha malisho na ardhi ya kilimo inayozidi kuadimika na pia kuigawa kihaki bajeti ya taifa.

Ban Ki-Moon wakati wa ziara yake ya siku nne nchini Sudan,aliweza kujionea mwenyewe uhalali wa madai hayo.Mji mkuu Khartoum unafumuka.Kreni zimesongamana kwenye viwanja vya ujenzi na majengo ya kisasa yanatazamana.Kasri jipya la rais linajengwa kwa msaada wa mkopo uliotolewa na China bila ya kutozwa riba.Uchumi unakua kwa zaidi ya asilimia 10.

Lakini hali ya mambo ni tofauti kabisa katika mji mkuu wa mkoani,El-Fasher ulio kaskazini ya Darfur.Barabara mbaya zinageukakuwa njia za matope wakati wa msimu wa mvua;kuna nyumba za kimasikini na kando ya barabara zipo kambi za wakimbizi zilizojaa watu kupindukia kiasi.

Bila shaka,majadiliano yatakayofanywa Libya mwezi ujao,yatakuwa magumu.Lakini Wasudani mwisho wa mwaka 2004,walifanikiwa kuanzisha usawa wa aina fulani.Wakati huo serikali ya Khartoum na waasi wa kusini ya Sudan walitia saini makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miaka 20.Makubaliano hayo ya amani yamedumu hadi hivi sasa.

Hata hivyo ni dhahiri kuwa mgogoro wa Darfur unaoendelea zaidi ya miaka minne,hauwezi kumalizwa kwa kupeleka tu kikosi kikubwa cha Umoja wa Mataifa kusimamia amani,ikiwa makundi 19 mbali mbali ya waasi na wanamgambo,yataendelea kupigana.