1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya kuundwa Ugiriki, Papandreou kujiuzulu

7 Novemba 2011

Ofisi ya Rais nchini Ugiriki imesema kwamba, waziri mkuu wa nchi hiyo na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani wamefikia makubaliano ya mwanzo juu ya uundaji wa serikali ya muda.

https://p.dw.com/p/1366y
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.Picha: dapd

Waziri Mkuu George Papandreou amekubali sharti la Antonis Samaras la kuwachia madaraka, na sasa viongozi hao wawili wanakutana leo (97.06.2011), kupanga muundo wa serikali hiyo, kumaliza mkwamo wa kisiasa ulioilemaza kabisa nchi hiyo. Jukumu kubwa la serikali hiyo ni kuhakikisha kuwa, mpango wa Umoja wa Ulaya kuinusuru Ugiriki kufilisika unapita Bungeni, kabla ya kujiuzulu kwake kwa ajili ya uchaguzi wa mapema.

Mpango huo wa Umoja wa Ulaya, unalazimisha hatua zaidi za kubana mkanda kwa Ugiriki, ili kufutiwa sehemu ya deni lake na kupata mkopo zaidi. Wiki iliyopita, mpango huo ulijikuta mashakani, baada ya Papandreou kutangaza kwamba angeliutishia kura ya maoni. Baadaye aliuondoa uamuzi huo.

Merkel atangaza punguzo la kodi

Kansela Angela Merkel (kulia) na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble.
Kansela Angela Merkel (kulia) na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble.Picha: dapd

Katika hatua nyengine kuhusiana na mgogoro wa madeni barani Ulaya, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kwamba chama chake cha Christian Democrats na washirika wake wamekubaliana juu ya punguzo la kodi kwa Wajerumani, linalofikia euro bilioni sita kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2013.

Kansela Merkel amesema hiyo ni kama shukrani kwa walipa kodi wa Ujerumani kwa mzigo waliopaswa kuubeba kutokana na mgogoro wa madeni unaoendelea barani Ulaya. Amesema kuwa ukatwaji huo wa kodi utafanyika katika hatua mbili, ambapo wa kwanza wenye thamani ya euro bilioni mbili, utafanyika Januari mwaka 2013 ukiwa na lengo la kupunguza mzigo, kwa walipa kodi wa kipato cha kati. Awamu ya pili itakuwa Januari mwaka 2014, ukiwa na thamani ya euro bilioni nne. Sheria hii inapaswa kwanza kupitishwa na bunge.

Masoko yaporomoka

Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou (kushoto), Rais wa Ugiriki Karolos Papoulias (kati) na kiongozi wa upinzani, Antonis Samaras, wakizungumzia serikali mpya.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou (kushoto), Rais wa Ugiriki Karolos Papoulias (kati) na kiongozi wa upinzani, Antonis Samaras, wakizungumzia serikali mpya.Picha: dapd

Hata hivyo, masoko ya hisa duniani yameendelea kutikisika, licha ya kuwepo kwa uwezekano wa kuundwa kwa serikali mpya nchini Ugiriki. Hadi asubuhi hii, masoko barani Asia yalikuwa yako chini, ambapo soko la Nikkei nchini Japan, limeshuka kwa asilimia 0.45, huku lile la Australia, likishuka kwa asilimia 0.13.

Lakini faharasa ya soko la hisa la Marekani imepanda kidogo, baada ya Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou, na kiongozi wa upinzani, Antonis Samaras, kukubaliana juu ya uundwaji wa serikali mpya ya mpito, kupitisha mpango wa mkopo wa Umoja wa Ulaya. Papandreou na Samaras wamekuwa wakifanya kazi ngumu mwishoni mwa wiki kufikia makubaliano, kabla ya mawaziri wa fedha wa mataifa yanayotumia sarafu ya euro, kukutana mjini Brussels jioni ya leo.

Wakati huo huo, wawekezaji wameanza kuelekeza macho yao nchini Italia, wakiweka shinikizo kwa serikali ya nchi hiyo, kurejesha haraka imani ya masoko ya fedha. Italia inahofiwa kuwa nchi nyengine itakayohitaji msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya, kuinusuru isifilisike.

Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR

Mhariri: Josephat Charo