1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kansela Merkel yapata pigo kubwa

10 Mei 2010

Nchini Ujerumani,vyama vya CDU na FDP vimepata pigo kubwa katika uchaguzi uliofanywa siku ya Jumapili jimbo la North Rhine Westphalia.

https://p.dw.com/p/NKI6
Der nordrhein-westfaelische CDU Ministerpraesident Juergen Ruettgers spricht am Sonntag, 9. Mai 2010, in Duesseldorf, Nordrhein-Westfalen, zu seinen Parteimitgliedern. Die Buerger von NRW waren am Sonntag aufgerufen, einen neuen Landtag zu waehlen. (apn Photo/Roberto Pfeil) --- North Rhine-Westphalia's state governor Juergen Ruettgers talks to his Christian Democratic party, CDU, members in Duesseldorf, Germany, Sunday, May 9, 2010. North Rhine-Westphalia's citizen were called to elect an new state parliament today. (apn Photo/Roberto Pfeil)
Waziri Mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia, Juergen Ruettgers.Picha: AP

Serikali ya muungano wa vyama hivyo viwili maarufu kama muungano wa "nyeusi na manjano", imetimuliwa baada ya kuwa madarakani kwa awamu moja tu chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Jürgen Rüttgers wa chama cha kihafidhina CDU. Hiyo jana, chama hicho kimeweza kupata asilimia 34.6 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia. Kulinganishwa na uchaguzi uliopita katika mwaka 2005, chama hicho kimepoteza kiasi ya asilimia 10, wakati washirika wake FDP wamepata asilimia 6.7 yaani takriban kiwango kile kile cha mwaka 2005, lakini ni nusu ya kura walizojikingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.

Matokeo ya uchaguzi huo wa jimbo la North Rhein Westphalia yanatazamwa pia kama kipimo kwa serikali ya muungano wa CDU na FDP mjini Berlin inayoongozwa na Kansela Angela Merkel. Washindi dhahiri wa uchaguzi wa hiyo jana katika jimbo la North Rhine Westphalia, ni chama cha Kijani kilichojikingia zaidi ya asilimia 12 ya kura zilizopigwa katika jimbo lenye wakaazi wengi kabisa nchini Ujerumani. Na chama cha mrengo wa kushoto Die Linke, kwa mara ya kwanza, kinaingia katika bunge la Düsseldorf baada ya kushinda asilimia 5.6.

Majadiliano kuhusu serikali mpya itakayoundwa katika jimbo la North Rhine Westphalia yanafanywa leo hii. Vyama vya SPD na Kijani vingependa kutawala pamoja, lakini serikali hiyo itakuwa na uwingi wa kura moja tu katika bunge la Düsseldorf. Vyama hivyo vingeweza kupata wingi mkubwa kwa kushirikiana na chama cha Die Linke, lakini SPD na Kijani vinasita kushirikiana na chama hicho, kwa sababu ya sera zake kali za mrengo wa kushoto. Uwezekano wa tatu uliopo, ni kuunda serikali ya muungano mkubwa kati ya SPD na CDU.

Hiyo jana chama cha SPD, hakijaamini bahati yake, matokeo ya uchaguzi yalipoanza kutangazwa. Baada ya kushindwa vibaya miaka mitano iliyopita katika jimbo la North Rhine Westphalia, viongozi na wanachama wa SPD walisherehekea ushindi wao katika makao makuu ya SPD mjini Berlin. Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel alisema:

"Hatujawahi kushuhudia wala kusikia furaha kama hiyo kwa muda mrefu. Wakati umewadia kwa hali kama hiyo kujitokeza kama hivi sasa."

Der SPD-Vorsitzende Siegmar Gabriel spricht am Sonntag, 9. Mai 2010, in der SPD Parteizentrale in Berlin zu den ersten Prognosen der Landtagswahlen in Nordrhein-Westfalen. (apn Photo/Sebastian Willnow) --- Sigmar Gabriel, Chairman of Germany's Social Democratic Party, SPD, delivers a speech to comment the first prognosis of the state election in North Rhine-Westphalia, in Berlin, Sunday, May 9, 2010. (apn Photo/Sebastian Willnow)
Mwenyekiti wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel.Picha: AP

Kwa maoni ya Gabriel,wapiga kura katika jimbo la North Rhine Westphalia sio tu wamekiunga mkono chama cha SPD na mgombea wao Hannelore Kraft, bali pia wameipinga serikali kuu ya muungano wa CDU na FDP mjini Berlin.

Serikali yo yote ile itakayoundwa katika jimbo la North Rhine Westphalia, moja ni dhahiri - serikali kuu mjini Berlin imepoteza wingi wake katika baraza la waakilishi wa serikali za majimbo Bundesrat. Na hiyo itaathiri maamuzi muhimu yanayohitaji kuidhinishwa na Budesrat. Miongoni mwa mipango mikubwa inayongojewa kuamuliwa na serikali ya Kansela Merkel, ni pendekezo la kupunguza kodi ya mapato na kufanya mageuzi katika mfumo wa huduma za afya.

Mwandishi: Werkhäuser,Nina/ZPR/P.Martin

Imepitiwa na : M.Abdul-Rahman