1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya mpito kuundwa nchini Tunisia

26 Oktoba 2011

Chama cha kiislamu cha Ennahda chafanya mazungumzo na vyama vengine leo kuamua uwezekano wa kuunda serikali ya mpito nchini Tunisia.

https://p.dw.com/p/12zNa
Mkuu wa chama cha Annahda Rashed GannouchiPicha: DW

Kufuatia uchaguzi wa kwanza wa kihistoria kufanyika nchini Tunisia tangu kuanza kwa wimbi la mapinduzi ya kiraia katika nchi za kiarabu, Chama cha kiislamu cha Ennahda kilitangazwa kuongoza katika matokeo ya kura.

Ingawa chama hicho hakikupata kura za kutosha kubuni serikali peke yake, sasa kimeanza mazungumzo na vyama vengine ili kuangalia uwezekano wa kuunda serikali ya mpito nchini humo itakayoongoza nchi hiyo kwa njia ya kidemokrasia.

Chama cha Ennahda kimesema tayari kimechukua ushindi wa asilimia 40 ya viti 217 vinavopiganiwa ili kushughulikia mchakato mzima wa kutunga katiba mpya ya nchi hiyo.

Hatua ya chama cha Ennahda kushinda uchaguzi huo wa kihistoria na kufanya kazi pamoja na vyama vengine itaangaliwa kwa karibu na mataifa mengine ya kiarabu, ambapo vyama vengine vya kiislamu vinatarajiwa kumaliza uchaguzi wake hivi karibuni.

Puzzlebild Triptychon Tunesien Wahlen Flagge Dossierbild 2
Raia wa Tunisia wakipeperusha bendera ya nchi yao.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, sasa Mahir Larbi, mkuu wa chama kilichoibuka cha tatu katika uchaguzi huo, amesema ni lazima vyama vyote vishirikiane katika kupatikana demokrasia na amani ya kudumi nchini humo.

Waangalizi wa kura nchini Tunisia waliupongeza uchaguzi wa kihistoria uliofanyika siku ya jumapili na kusema ulikuwa huru na wa haki, licha ya kuwa na visa vya ghasia kufuatia maandamano ya kumuondoa rais wa zamani wa nchi hiyo, Zein el abidin Ben Ali, aliyeondoka na kukimbilia mafichoni nchini Saudi Arabia.

Chama Cha Ennahda, kupitia meneja wake wa kampeni, Abdel Hamid Jellasi, kimesema lengo lake kwa sasa ni kuunda serikali ya muungano wa kitaifa na kamwe hawatakibagua chama chochote katika kuungana pamoja katika kuleta demokrasia nchini Tunisia.

Jelassi amsema chama hicho kilitengwa na kupigwa marufuku chini ya utawala wa rais wa zamani Zein El Abidin Ben Ali na kamwe hawatakibagua chama chochote katika kuufungua ukurasa mpya nchini Tunisia.

Chama cha Ennahda kinataka sheria ya kiislamu ijumuishwe katika mojawapo ya sheria nchini humo.

Mwandishi Amina Abubakar/APE

Mhariri Othman Miraji