1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya mpito Sudan Kusini kutoanza kama ilivyopangwa

22 Januari 2016

Serikali ya mpito ya Sudan Kusini iliyotarajiwa kuanza rasmi shughuli zake hii leo imetangaza kuakhirisha mpango huo.

https://p.dw.com/p/1Hi8q
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Muller

Msemaji wa serikali Atenya Wek Ateny, amethibitisha hayo na ameweka wazi kwamba takriban thuluthi mbili ya masuala ya kiserikali yataendeshwa kama ilivyokuwa huko nyuma. Serikali hiyo ya mpito ya Umoja wa Kitaifa ilitarajiwa kuundwa leo (22.01.2016) ili kumaliza mgogoro wa miaka miwili uliosababisha zaidi ya watu 15,000 kuuwawa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa ikitarajiwa kuundwa na kuanza kazi leo ikihusisha mawaziri 30.

Kuundwa kwa serikali hiyo ni mchakato uliokwenda sambamba na makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na viongozi wawili wanaozozana Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar kufuatia shinikizo la kimataifa mnamo mwezi Agosti mwaka jana.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha watu zaidi ya milioni mbili kuachawa bila makaazi vilihusisha mapambano kati ya wanajeshi wa serikali ya Rais Kiir na waasi wanaomuunga mkono mpinzani wake kisiasa Riek Machar.

Siku ya kihistoria

Kimsingi leo ilikuwa siku muhimu iliyotarajiwa kuweka msingi wa kupigwa hatua katika historia ya taifa hilo la Sudan Kusini ambalo limeshuhudia miaka miwili ya mapigano kati ya pande hizo mbili hasimu.

Raia zaidi ya milioni 12 wa nchi hiyo walitarajia kuiona serikali mpya ya mpito itakayozijumuisha pande zote huku Salva Kiir akiendelea kushikilia nafasi yake kama rais na Machar kurudishwa katika nafasi yake ya zamani, yaani makamu wa rais.

Serikali hiyo ya mawaziri 30 ikitarajiwa kwamba itajumuisha watu sita walioteuliwa na Rais Kiir huku wengine 10 wakiteuliwa na Machar na wawili wakiteuliwa kutoka upande wa wale waliokuwa wamezuiliwa jela na wengine wawili wakiteuliwa na muungano wa vyama vidogo vya kisiasa nchini Sudan Kusini.

Baadhi ya viongozi wanachama wa IGAD
Baadhi ya viongozi wanachama wa IGADPicha: ZACHARIAS ABUBEKER/AFP/Getty Images

Ama kwa upande mwingine, ikitazamiwa kwamba baada ya mchakato mwishoni mwa miezi 30 jeshi la Sudan Kusini ambalo kwa hivi sasa limegawikaa pande mbili, upande mmoja ukiegemea kambi ya Rais Kiir na upande wa pili wakiwa watiifu wa Machar, walitarajiwa kuunganishwa hatua ambayo itafuatiwa na mchakato wa kuitishwa uchaguzi wa rais na Bunge.

Awali Rais Kiir akizungumza kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, aliwataka wananchi wa taifa hilo kumpokea Riek Machar na wenzake 600 kwa mikono miwili wakati wakiwasili nchini humo.

''Nawatolea mwito nyote kuwakaribisha kaka zenu na dada zenu, watoto wenu wa kike kwa wa kiuume pindi wakirejea nchini. Wakaribisheni kwa mikono mwili, mridhiane na kusameheeana, msahau yaliyopita na kuanzisha ukurasa mpya, mjenge hali ya kuaminiana na imani miongoni mwenu na muishi kwa amani na upendo,'' alisema Rais Kiir.

Rais Kiir azungumzia vipaumbele

Kiongozi huyo aliendelea kusisitiza, ''Tunapojiandaa kuzindua serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa vipaumbele vyetu vya mwanzo vitakuwa ni kutafuta utekelezaji wa kudumu wa kusitisha mapigano pamoja na kujenga amani na kurekebisha shule zilizoharibiwa kwa vita pamoja na mahospitali. Kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi ya kunywa na kurudisha katika hali ya kawaida maeneo yaliyoathiriwa na vita.''

Ikumbukwe kwamba yote hayo yanafuatia makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Jumuiya ya ushirikiano katika kanda ya Afrika Mashariki-IGAD na ambayo yaliridhiwa na kutiwa saini na Rais Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar, Agosti mwaka jana hatua iliyofungua njia ya kupatikana mwafaka wa kuundwa serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa. Utekelezwaji wa makubaliano huo unafuatiliwa na aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae.

Hayo yanajiri wakati ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeleeza kuwa majeshi ya serikali ya Sudan Kusini yaliwashikilia wanawake kama watumwa wa ngono, huku yakivamia raia nje ya kambi za Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mamia ya watu, wakiwemo wanawake wajawazito na wasichana wadogo walibakwa kwenye jimbo la Unity na wanajeshi wa ama pande zote mbili. Hata hivyo, serikali ya Sudan Kusini imekanusha taarifa hizo za ubakaji na uhalifu mwingine.

Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef
Source: Africa Link/APE