1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya pande tatu kisiwani Madagascar

Oumilkher Hamidou7 Oktoba 2009

Pandea zinazohasimiana katika kisiwa cha bahari ya Hindi cha Madagascar zaunga mkono serikali ya pande tatu iongozwe na Andry Rajoelina

https://p.dw.com/p/K0iS
Andry Rajoelina anaendelea kudhibiti hatamu za uongozi kisiwani MadagaascarPicha: picture alliance/dpa

Umoja wa Afrika umefanikiwa kuzitanabahisha pande tatu zinazohasimiana kisiwani Madagascar zikubaliane kuunda utawala wa pande tatu,utakaoongozwa na rais wa sasa Andry Rajoelina.

Mtangulizi wake,Marc Ravalomanana,aliyeng'olewa madarakani kwa msaada wa baadhi ya wanajeshi na Andry Rajoelina amekiri mpinzani wake aendelee kuwepo madarakani,kwa sharti lakini,hatogombea kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa hivi karibuni.Haijulikani lakini kwasasa kama Rajoelina amekubali sharti hilo au la.

"Rais ni Andry Rajoelina,makamo wa rais ni Emmanuel Rakotovahiny na waziri mkuu ni Eugene Mangalaza" amesema Ange Andrianarisoa ambae ndie mkuu wa ujumbe mmojawapo wa wabuki waliohudhuria mazungumzo hayo ya amani.

Kabla ya hapo,Umoja wa Afrika uliwasihi wakuu wa pande zinazohasimiana,warejee katika meza ya mazungumzo ili kuunda serikali ya ridhaa kama ilivyotajwa katika makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa mjini Maputo nchini Mosambik,mwezi Agosti mwaka huu.

Kuundwa serikali hiyo ya ridhaa kutasaidia kumaliza wasi wasi uliozuka baada ya meya huyo kijana wa jiji la Antananarivo,Andry Rajoelina kunyakua madaraka kwa msaada wa baadhi ya wanajeshi March mwaka huu na kupelekea kisiwa hicho cha bahari ya hindi kutengwa na jumuia ya kimataifa.

Mjumbe wa Umoja wa Afrika anaeshughulikia mzozo wa Madagascar,Ablassé Ouédraogo amesema makubaliano ya jana jumanne ni hatua ya mwanzo katika utaratibu wa kuheshimiwa katiba.

"Kilichofikiwa hapa ni hatua ya mwanzo tuu katika kuanzishwa kipindi cha mpito na kutekeleza makubaliano ya maputo."Amesema.

Ameongeza kusema hata hivyo kwamba Marc Ravalomanana ameshurutisha kusalia Rajoelina kama rais wa muda na kutolewa ahadi kwamba mpinzani wake hatopigania wadhifa wa rais-sharti ambalo,kwa mujibu wa mjumbe wa Umoja wa Afrika,halijatajwa katika makubaliano ya Maputo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Afrika,Jean Ping amesema tunanukuu"Makubaliano ya maputo hayana badala."Makubaliano hayo yametiwa saini na Andry Rajoelina,Marc Ravalomanana na marais wawili wa zamani wa Madagascar,Didier Ratsiraka na Albert Zafy.

Jean Ping ameonya vikwazo vya kimataifa vinaweza kuselelea .Amekwepa pia kusema lini Madagascar itaruhusiwa upya kujiunga na Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afriika-SADC.

"Baadhi ya hatua zitaendelea ,ikiwa hakuna nia ya kumaliza mzozo" amesema katibu mkuu wa Umoja wa Afrika,Jean Ping na kusisitiza,misaada ya kimataifa iliyozuwiliwa haitotolewa si mpaka hali inarejea upya kua ya kawaida."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman