1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Papandreou yanusurika

22 Juni 2011

Serikali ya Ugiriki imo mbioni kujaribu kuidhinisha mpango wa kubana matumizi yake, baada ya Waziri Mkuu George Papandreou kuungwa mkono katika kura ya imani iliyopigwa bungeni jana usiku.

https://p.dw.com/p/RV5t
In this image taken from TV, Greek Prime Minister George Papandreou, talks to the nation in a live TV broadcast Wednesday June 15, 2011, in Athens, Greece. Papandreou said that coalition talks with opposition failed, but he would not resign and that he would reshuffle the government Cabinet. (Foto:TV pool/AP/dapd)
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George PapandreouPicha: dapd

Serikali ya Ugiriki imenusurika baada ya kuungwa mkono kwa kura 155 bungeni na hivyo imeruka kiunzi cha mwanzo katika jitahada ya kupata mkopo wa dharura ili isijekufilisika. Waziri Mkuu Papaendreou aliungwa mkono na wabunge wa chama chake cha Pasok, licha ya wengi wao hapo awali kuukosoa vikali mpango wake wa kubana matumizi ya serikali.

Kuambatana na mpango huo, serikali inatazamia kupunguza matumizi, kupandisha kodi na kuuza mali yake ili iweze kupata sehemu ya msaada wa fedha uliokubaliwa na Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF mwaka uliopita. Waziri mpya wa fedha Evangelos Venizelos jana usiku aliwaambia wabunge:

"Sisi sio wabaya wa Ulaya. Tuna ari na sasa tunapitia wakati mgumu. Lakini katika historia yetu mara nyingi tumeweza kuudhibiti wakati mgumu. Tutathibitisha kuwa kizazi chetu kitashinda vita hivi."

Hivyo ni vita vya kupambana na madeni; na silaha ni mpango wa kubana matumizi unaozusha mabishano makali nchini humo. Maelfu ya watu walikusanyika nje ya bunge kuupinga mpango huo wakilalamika kuwa masikini ndio wanaobeba mzigo na sio matajiri. Waandamanaji hao wanahisi kuwa vyama vikuu vilivyo bungeni na hata vyama vya upinzani, haviwakilishi maslahi ya umma huo.

Hata hivyo, serikali ya Papandreou iliyopangwa upya hivi karibuni, inataka kuidhinisha mpango huo bungeni hadi Juni 28, ili iweze kupata mkopo mpya kutoka Umoja wa Ulaya na IMF. Baadae baraza la mawaziri litapitisha sheria zinazohitajiwa ili kuweza kuutekeleza mpango huo na hivyo kupata msaada wa Euro bilioni 12 na kujiepusha kufilisika.

Hatua za kubana matumizi ni masharti ya kupewa fungu jipya la fedha kutoka jumla ya Euro bilioni 110 zilizokubaliwa na Umoja wa Ulaya na IMF katika mpango mpya wa kupunguza matumizi kwa miaka mitano ijayo. Bila ya mkopo huo, Ugiriki itaishiwa na fedha zake mwezi ujao na maafisa wa serikali wana hofu kuwa kufilisika kwa Ugiriki kutaathiri pia mfumo wa kiuchumi kote duniani.

Mwandishi: Bormann,Thomas/ZPR/afpe,rtre

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed