1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Somalia yasaini makubaliano ya amani na mahasimu wake wakuu.

Mohamed Dahman10 Juni 2008

Serikali ya mpito ya Somalia na mahasimu wake wakuu wa kisiasa wametia saini makubaliano ya miezi mitatu ya kusitisha uhasama katika mazungumzo ya amani yaliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa nchini Djibouti.

https://p.dw.com/p/EGhT
Wanajeshi wa serikali ya mpito wakiwa kwenye doria na silaha nzito katika mitaa ya mji mkuu wa Somalia Mogadishu.Picha: AP

Makubaliano hayo yalifokiwa hapo jana pia yanatowa wito wa kuwekwa kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kuleta utulivu nchini humo.

Kwa mujibu wa maudhui ya makubaliano hayo yaliotumwa kwa waandishi wa habari usitishaji wa malumbano ya kijeshi unapaswa kuanza kutekelezwa katika ardhi yote ya Somalia siku 30 baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yatatekelezwa katika kipindi cha awali cha siku 90 na baadae yataongezewa muda.

Waziri Mkuu wa Somalia Nur Hassan Hussein na Kiongozi wa Muungano wa Kuikombowa Upya Somalia Sheikh Sharif Ahmed wamesaini makubaliano hayo katika sherehe zilizoshuhudiwa na Umoja wa Waarabu,Umoja wa Afrika,Umoja nwa wa Ulaya,Marekani na Saudi Arabia.

Muungano wa Kuikombowa Upya Somalia ni kundi la upinzani linadhobitiwa na Waislamu wa itikadi kali lenye makao yake katika mji mkuu wa Eritrea Asmara.

Wakati baadhi ya viongozi wa itikadi kali za Kiislam na viongozi wa kikabila wenye ushawishi walijiunga na mazungumzo hayo Waislamu wengine wa itikadi kali wenye kichwa ngumu wanasisitiza kwamba mazungumzo hayo yalikuwa ya upendeleo na wameshiklia wito wao wa kuondolewa kwa vikosi vya Ethiopia kutoka Somalia kabla ya kufanyika kwa mazungumzo yoyote yale.

Katika makubaliano hayo mahasimu hao wameiomba Umoja wa Mataifa kuweka wanajeshi wa kulinda amani kutoka nchi zilizo rafiki kwa Somalia na kutoziingiza nchi jirani na Somalia katika kipindi kisichozidi siku 120 kutoka siku ya kuanza kutekelezwa kwa usitishaji huo wa mapigano.

Katika kipindi hicho hicho serikali itachukuwa hatua kwa mujibu wa uamuzi ambao tayari umepitishwa na Ethiopia wa kuondowa vikosi vyake kutoka Somalia baada ya kuwekwa kwa wanajeshi wa kutosha wa Umoja wa Mataifa.

Pia wamekubaliana kuunda Kamati ya Usalama ya Pamoja chini ya uenyekiti wa Umoja wa Mataifa katika kipindi kisichozidi siku 15 za kutiwa saini kwa makubaliano hayo kusimamia utekelezaji wa usitishaji wa mapigano.Pia watakutana hapo tarehe 30 mwezi wa Julai kujadili ushirikiano wa kisiasa,sheria na usuluhishi.

Matumaini ya kufikiwa makubaliano katika mazungumzo hayo ya Djibouti yalififia baada ya wapinzani vichwa ngumu kuwakebehi viongozi wengine wa upinzani walioshiriki mazungumzo hayo.

Pia kwa siku kadhaa wajumbe walikuwa wamegoma kukutana ana kwa ana kujadili njia za kukomesha mzozo wa takriban miaka 18 na walikubali tu kukutana moja kwa moja hapo jana wakati wa kusaini makubaliano hayo.

Wakati wapinzani vichwa ngumu walioko uhamishoni na waasi walioko ndani ya Somalia wameyapuzilia mbali mazungumzo hayo yalioongozwa na Umoja wa Mataifa nchini Djibouti bado haiko dhahir vipi yataweza kutekelezeka nchini Somalia kwenyewe.

Wimbi la umwagaji damu nchini Somalia limechochea maafa ya kibinaadamu ambayo wafanyakazi wa misaada wanasema yanaweza kuwa mabaya kabisa barani Afrika kutokana na kuwepo kwa takriban wakimbizi milioni moja katika taifa hilo lililokumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tokea kupinduliwa kwa dikteta wa kijeshi Mohamed Siad Bare hapo mwaka 1991 kulikofanywa na wababe wa vita.