1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Sudan na kundi la waasi la LJM watiliana saini

Kabogo Grace Patricia18 Machi 2010

Makubaliano hayo yamefikiwa huko Doha, Qatar na yatahusu suala la kusitisha mapigano na kufanyika mazungumzo mengine.

https://p.dw.com/p/MW9Z
Rais Omar al-Bashir wa Sudan.Picha: picture alliance / abaca

Serikali ya Sudan na kundi la waasi la Darfur -Chama cha  Ukombozi na Haki, Liberation and Justice Movement-LJM leo wametiliana saini mkataba wa amani wakati ambapo mazungumzo baina ya serikali na kundi kubwa jingine la waasi la chama cha haki na usawa,Justice and Equality Movement-JEM yakionekana kuzorota. Makubaliano ya kusitisha mapigano na kufanyika mazungumzo yamesainiwa huko Doha, Qatar kati ya mshauri wa Rais Omar al-Bashir, Ghazib Salahuddin na kiongozi wa kundi la waasi la Liberation and Justice Movement-LJM, El-Tijani El-Sissi.

Makamu wa Rais wa Sudan, Ali Osman Taha aliyehudhuria sherehe hizo za kutia saini amesema hiyo ni hatua muhimu ambayo itaifanya serikali ya nchi hiyo kuongeza kasi katika juhudi za kupatikana amani katika jimbo la Darfur. Osman Taha amesema serikali ya Sudan inajizatiti katika kushinikiza kufanyika mazungumzo ya amani kufuatia makubaliano yaliyofikiwa. Makamu huyo wa rais wa Sudan amevitolea mwito vyama vyote pamoja na kundi la Justice and Equality Movement-JEM, kushiriki katika mazungumzo ya dhati kwa lengo la kukamilisha taratibu zote za kufikia makubaliano ya mwisho.

Makubaliano hayo kati ya serikali ya Sudan na kundi hilo lililo chini ya mwamvuli wa makundi ya waasi yaliyojitenga yamefanyika ikiwa ni wiki kadhaa baada ya serikali kutiliana saini mkataba kama huu na kundi kubwa la waasi la JEM. Hata hivyo makubaliano haya yaliyofikiwa hii leo yamepuuzwa na kundi la JEM, likisema kuwa kundi la LJM halina jeshi, lakini afisa wa ngazi ya juu wa JEM, Al-Tahir al-Feki ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kundi lake litayaunga mkono makubaliano hayo mapya kama makundi ya waasi yaliyo chini ya LJM yatakubali kujiunga na vikosi vyake vya jeshi na kuafikiana na serikali ya Sudan kama kundi moja.

Makubaliano kati ya serikali ya Sudan na kundi la JEM yaliyofikiwa mwezi uliopita yakiwa kama hatua muhimu kuelekea kupatikana amani katika jimbo la Darfur yamekuwa katika wakati mgumu. Viongozi wa Sudan waliwakamata tena wanachama 15 wa kundi la JEM siku ya Jumatano baada ya kuwaachia huru kufuatia makubaliano hayo ambayo yanasita sita. Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Hamad bin Jaseem al-Thani ametahadharisha kuwa makubaliano mapya yako mbali ili kukamilishwa. Sheikh Hamad anasema ana matumaini kuwa makubaliano hayo yataendelea kwa kuwa wana kazi kubwa katika kuyakamilisha.

Sheikh Hamad ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Qatar, amesema kuwa kundi la JEM ni mshirika muhimu katika mazungumzo hayo ya amani. Kundi nyingine muhimu la waasi la Sudan Liberation Army-SLA linaloongozwa na Abdelwahid Nur hadi sasa limekataa kushiriki katika mazungumzo yoyote yale na serikali ya Sudan. Mwanzoni mwa mwezi huu kundi hilo la SLA lilikuwa katika mapigano na vikosi vya jeshi la serikali katika eneo la Jebel Marra

Aidha mwanzoni mwa mezi huu, mjumbe maalum wa Marekani nchini Sudan, Scott Gration alisema kuwa ni muhimu kuharakisha mikakati ya kuelekea katika amani kabla matatizo ya Darfur hajayafunikwa na masuala ya uchaguzi. Sudan inatarajia kufanya uchaguzi wa urais, wabunge na majimbo mwezi ujao wa Aprili, huo ukiwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi katika kipindi cha robo karne na tukio muhimu la kihistoria tangu kutekelezwa kwa makubaliano ya amani kati ya kaskazini na kusini ya mwaka 2005.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman