1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yakanusha kufanya mauaji mengine ya maangamizi

7 Juni 2012

Serikali ya Syria imekanusha kufanyika kwa mauaji mengine ya maangamizi katika mkoa wa katikati wa Hama ambako ripoti zinasema kiasi ya watu 100 waliuawa hapo jana.

https://p.dw.com/p/159vu
Wanafunzi wakiigiza mauaji ya maangamizi ya Houla.
Wanafunzi wakiigiza mauaji ya maangamizi ya Houla.Picha: Reuters

Taarifa ya serikali iliyotolewa leo kupitia televisheni ya taifa imesema kilichotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari juu ya tukio la jana kwenye mji wa Al-Kubeir ulio kwenye mkoa wa Hama hakikuwa sahihi.

Badala yake, taarifa hiyo imesema, kundi la magaidi lilifanya uhalifu uliopelekea vifo vya watu tisa. Shirika la Habari la AFP lilinukuu Baraza la Kitaifa la Syria, likisema vikosi vitiifu kwa Rais Bashar Assad vimewaua watu 100.

Vyanzo vingine vya habari, likiwemo Shirika la Haki za Binaadamu la Syria na wanaharakati wa upinzani, vimeripoti kutokea kwa mauaji kwenye eneo hilo hilo la al-Kubeir huku vikisema idadi ya waliouawa ni 87.

Wanamgambo wa Sabiha wanaoiunga mkono serikali wanatajwa kuhusika. Picha za video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha miili kadhaa ikiwa imezongwa nguo za kuihifadhi.

Mauaji ya maangamizi katika eneo la Houla wiki mwishoni mwa mwezi uliopita yalisababisha lawama kali dhidi ya utawala wa Rais Assad. Katika mauaji hayo, zaidi ya watu 100, wengi wao wanawake na watoto waliuawa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman