1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yawaachilia huru wafungwa 755

28 Desemba 2011

Syria imesema leo kuwa imewaachilia huru wafungwa 755 waliohusika katika maandamano ya kuipinga serikali, huku waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu Arab League, wakiyazuru maeneo yanayokabiliwa na ghasia.

https://p.dw.com/p/13b2Y
Waandamanaji nchini Syria
Waandamanaji nchini SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Televisheni ya kitaifa imesema leo kuwa wafungwa hao 755 waliohusika kwenye matukio ya hivi karibuni nchini Syria na ambao hawakuwa na damu za Wasyria mikononi mwao wamewachiliwa huru kutoka gerezani.

Kuwaachilia huru wafungwa ni mojawapo ya masharti muhimu ya mpango wa umoja wan chi za Kiarabu ulioidhishwa na Syria mwezi uliopita wa kumaliza mzozo unaoshuhudiwa nchini humo. Mkataba huo pia unataka kusitishwa kwa ukandamizaji unaofanywa dhidi ya waandamanaji wanaoiunga mkono demokrasia. Kulingana na polisi nchini Syria, zaidi ya wafungwa 4,300 waliokamatwa wakati wa misako ya vikosi vya usalama vya serikali dhidi ya wapinzani waliwachiliwa huru mwezi Novemba.

Waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu leo walizuru maeneo muhimu ambayo yemekuwa vitovu vya ghasia nchini Syria, huku mataifa makuu ulimwenguni yakiitaka serikali ya nchi hiyo iwawezeshe kuzuru maeneo hayo na kufichua ukweli kuhusu ukandamizaji unaofanywa dhidi ya upinzani.

Shirika la haki za binadam la Syrian Observatory for Human Rights limesema umwagikaji zaidi wa damu pia uliripotiwa, huku wanajeshi walioitoroka serikali wakiwauwa wanajeshi wanne wa serikali ya Syria katika mkoa wa kusini wa Daraa, na raia mmoja akapigwa risasi na kuuwawa katika mji wa Homs. Shutuma kuwa utawala unajaribu kuficha ukweli kwa waangalizi hao zilisisitizwa na Ufaransa, ambayo ilidai kuwa kundi hilo halikukubaliwa kuona kile kinachotendeka katika mji wa ghasia wa Homs, huku ukandamizaji ukiendelea katika eneo hilo.

Waangalizi hao wanatarajiwa kuzuru Daraa, ambao umekuwa kitovu kikubwa cha maandamano ya miezi tisa ya kuupinga utawala, mikoa ya kaskazini ya Hama na Idlib na maeneo ya karibu na mji mkuu, Damascus, ili kujaribu kufanya uchunguzi wao.

Kiongozi wa kundi la waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu nchini Syria, Mohamed Ahmed Mustafa Al-Dabi
Kiongozi wa kundi la waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu nchini Syria, Mohamed Ahmed Mustafa Al-DabiPicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa ujumbe huo wa jumuiya ya Kiarabu ambaye ni jenerali mkongwe wa jeshi la Sudan, Mohammed Ahmed Mustafa al-Dabi, amesema ziara ya waangalizi hao katika eneo la Homs ilikuwa ya kufana na akaongeza kuwa waangalizi zaidi watajiunga na ujumbe huo ambao kwa sasa una waangalizi 65.

Waziri wa mambo ya  nchi za nje ya Ufaransa, Benard Valero, amesema ziara hiyo ya Homs ilikuwa fupi mno na haikufichua mambo mengi. Amesema idadi ndogo ya waangalizi haikuweza kuzuia ukandamizaji unaoendelea katika mji huo ambako maandamano yalikabiliwa kwa nguvu kupita kiasi na kusababisha vifo vya watu 10. Urusi na Marekani pamoja na shirika la haki za binadam Human Rights Watch ni miongoni mwa wale wanaoitaka Syria kushirikiana na waangalizi hao kuhakikisha amani  nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Miraji Othman