1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya umoja wa kitaifa mashakani Zanzibar

Mohammed Khelef
15 Novemba 2022

Wakati mshirika mdogo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar, chama cha ACT Wazalendo, kikisubiriwa kuamuwa hatima ya serikali hiyo, vyama tisa ya upinzani vimekikosowa vikali chama hicho.

https://p.dw.com/p/4JXk8
Sansibar Inauguration Präsident Hussein Ali Mwinyi  Vizepräsident Othman Masoud Othman
Picha: Glenn Carnell/State House Zanzibar

Wakizungumza na waandishi wa habari, wanasiasa hao walisema mbali na kupongeza kuteuliwa kwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Thabit Faina, wamesifia uchaguzi wa mwaka 2020 wakidai kuwa ulifanyika kwa uwazi na uhuru na kutaka maamuzi ya Rais Hussein Mwinyikumteuwa tena Faina kutoingiliwa.

Hata hivyo, Ameir Hassan Ameir kutoka chama cha Demokrasia Makini, ambaye ndiye aliyeongoza mkutano huo ulioandaliwa kwenye jengo la zamani la Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni, Mjini Unguja, alisema alisema Rais Mwinyi hakufanya makosa kwenye uteuzi kwa kuwa ana mamlaka ya kuteuwa na kutengua kama apendavyo.

"Kwanza na sisi tunalaani hii kauli ambayo ACT Wazalendo wametowa kwa umma. Tunailaani kwa kuwa tunaona haina mustakabali mwema kwa Zanzibar. Hii ni kauli ya kibinafsi."

Itakumbukwa kwamba uchaguzi wa mwaka 2020 uliozaa serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Mwinyi ulitajwa kuwa mbaya kuliko yote iliyowahi kufanyika tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na vyama vikuu vya upinzani, kwa mujibu wa rikodi wa chama cha ACT Wazalendo.

ACT Wazalendo yapinga uteuzi

Sansibar Inauguration Präsident Hussein Ali Mwinyi  Vizepräsident Othman Masoud Othman
Rais Hussein Mwinyi wa Zanzibar kutoka chama cha CCM (kushoto) akimuapisha makamu wake wa kwanza, Othman Masoud kutoka chama cha ACT Wazalendo.Picha: Glenn Carnell/State House Zanzibar

Wiki iliyopita, ACT Wazalendo ilitoa tamko la kupinga uteuzi wa Thabit Faina kuwa tena mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa madai kwamba alichangia kuharibu uchaguzi huo ambao ulikumbwa na malalamiko mengi ya kiutendaji na ikataka kwanza asiapishwe.

"...vitendo cha Bwana Faina vilikuwa vya uhalifu wa wazi na makosa makubwa ya kutumia vibaya nafasi yake jambo ambalo ni kosa chini ya kifungu cha 53 cha Sheria za Zanzibar ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi..." ilisema sehemu ya tamko hilo.

Lakini wakizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, wanasiasa kutoka vyama tisa visivyokuwa na uwakilishi kwenye chombo chochote walisema wanaungana na Rais Mwinyi na wako naye kwa lolote lile.

Chadema na ACT walaani kupigwa kwa kada wa CCM

Kwa upande wake, chama kikuu cha upinzani ambacho si sehemu ya vyama hivyo tisa, CHADEMA, ilitowa waraka ukitaja kusikitishwa na uteuzi wa Bwana Faina huku wakimsihi Rais Mwinyi "kuendeleza kauli zake za maridhiano bila ya kukubali kutia doa dhamira yake ya umoja na mshikamano kwa Wazanzibari."

Mbali na chama cha Demokrasia Makini, vyama vingine vilivyoshiriki kwenye kuandaa na kutoa tamko la kuungana na Rais Mwinyi ni SAU, NLD, TLP, UDP, CCK, UMD na UPDP.

Imeandikwa na Salma Said/DW Zanzibar