1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Venezuela na upinzani wamerudi kwenye mazungumzo

4 Septemba 2021

Serikali ya Maduro imeomba kuondolewa vikwazo vya kimataifa, wakati upinzani unataka uchaguzi huru na wa haki. Taifa hilo la Amerika Kusini limekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu 2019.

https://p.dw.com/p/3zv38
Mexiko City | Politische Zusammenarbeit | Mexico und Venezuela
Picha: Marco Ugarte/AP Photo/picture alliance

Wajumbe kutoka serikali ya Venezuela na upande wa upinzani wameanza tena mazungumzo huko Mexico City Ijumaa, huku pande hizo mbili zikitarajia kupata suluhisho la kumaliza mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Lakini Rais wa Venezuela Nicolas Maduro wala kiongozi wa upinzani Juan Guaido hawakuhudhuria mkutano huo wa Mexico.

Pande hizo mbili zinadai nini?

Maduro ametaka kuondolewa vikwazo vya kimataifa alivyowekewa pamoja na kuutaka upinzani kutambua utawala wa serikali yake iliyo madarakani.

Upinzani kwa upande wake unataka kufanyike uchaguzi ulio huru na wa haki.

Soma zaidi:Maduro asema Venezuela haitasalimu kutokana na vitisho

"Lengo letu ni kufikia makubaliano ambayo yatasuluhisha mzozo kupitia uchaguzi wa urais na bunge ulio huru na wa haki," amesema Guaido katikia vidio iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Sote tunajua kuwa kwa hivi sasa hakuna mchakato wa uchaguzi ulio huru na wa haki nchini Venezuela. Ndio sababu tuko Mexico. Tunapigania kupata uhakika wa hilo," ameongeza Guaido.

Mazungumzo hayo yanadhaminiwa na serikali ya Mexico chini ya uongozi wa Rais Andres Manuel Obrador huku upatanishi ukifanywa na Norway. Obrador hata hivyo amewahi kuashiria kumuunga mkono Maduro.

Duru hiyo ya mazunguzo inatarajiwa kukamilika Jumatatu.

Mazungumzo hayo ya Mexico yalianza mwezi uliopita, na serikali pamoja na wajumbe wa upinzani walitia saini hati ya makubaliano wakati wa hafla ya ufunguzi.

Gespräche zwischen Venezuela und Mexiko
Mazungumzo kati ya serikali ya Venezuela na upinzani, MexicoPicha: Marco Ugarte/AP/picture alliance

Maridhiano yaliowezesha mazungumzo

Kila upande uliridhia masharti ya mwenzake ili mazungumzo yaweze kusonga mbele.

Serikali ilimuachilia huru kutoka gerezani kiongozi wa upinzani Freddy Guevara mwezi uliopita, huku upinzani umeahidi wiki hii kushiriki katika uchaguzi ujao wa manispaa. Upinzani umekubali kushiriki uchaguzi baada ya kuuogomea kwa miaka mitatu.

Soma zaidi: Upinzani Venezuela utashiriki uchaguzi wa mikoa

Kufuatia uchaguzi wa rais wa 2019, kulizuka mvutano kati ya Maduro na Guaido, huku kila mmoja akidai ushindi na kujitangaza kiongozi halali wa Venezuela.

Maduro aliungwa mkono na mataifa kama Urusi, China na Uturuki. Wakati Guaido aliungwa mkono na mataifa ya Magharibi kama vile Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Mazungumzo ya nyuma kati ya pande hizo mbili yaliyofayika Barbados 2019 na Dominican Republic 2018 yaliyshindwa kuzaa matunda na kusuluhisha mkwamo wa kisiasa wa Venezuela.

Uchumi wa Venezuela umeporomoka tangu 2013, huku nchi hiyo ikishuhudia mfumuko wa bei na upungufu wa chakula na mahitaji mengine muhimu.

Taifa hilo la Amerika Kusini pia limeshindwa kukabiliana na janga la virusi vya corona ambalo bado linaendelea, kwani madaktari na wahudumu wengi wa afya wameikimbia nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

wd/sms (AP, AFP, Reuters)