1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali yashutumu upinzani.

24 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cfds

Nairobi.

Serikali ya Kenya jana Jumapili imepuuzia madai mapya kuwa inapanga kufanya hila kuiba kura katika uchaguzi utakaofanyika wiki hii, na badala yake imeushutumu upande wa upinzani kwa kujaribu kupanga njama za kuzusha ghasia nchini humo.

Vyama viwili vikuu vya upinzani vimekishutumu chama cha PNU cha rais Mwai kibaki , ambaye yuko nyuma katika maoni ya wapiga kura , kwa kupanga mpango wa kuiba kura na kuibuka mshindi katika uchaguzi wa hapo Desemba 27.

Mgombea wa upinzani Raila Odinga ameandika barua kwa tume ya uchaguzi ya Kenya, kamishna wa polisi na ujumbe wa makundi ya kuangalia uchaguzi huo , akielezea mpango huo wa serikali.Maafisa wamesema kuwa licha ya kwamba Raila alitoa shutuma kama hizo mapema mwezi huu, mkuu wa tume ya uchaguzi Samuel Kivuitu amesema jana kuwa timu yake itafanya kile iwezalo kuzuwia wizi wa kura. Wakati huo huo polisi wamesema kuwa mtu mmoja ameuwawa katika jimbo la pwani siku ya Jumamosi, na kufikisha idadi ya watu waliouwawa katika ghasia kabla ya uchaguzi kufikia 73.