1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali yatofautiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu ICC

Sekione Kitojo19 Julai 2011

Serikali na vyama vya kijamii nchini Cote D'Ivoire vimegawanyika kuhusiana na kiwango cha uchunguzi unaotakiwa kufanywa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu nchini Cote D'Ivoire.

https://p.dw.com/p/11zkY
Majeshi yanayomuunga mkono rais wa Cote D'Ivoire Alassane Ouattara yakijitayarisha na mapambano mjini Abidjan.Picha: picture alliance / dpa

Serikali na vyama vya kijamii nchini Cote D'Ivoire vimegawanyika kuhusiana na kiwango cha uchunguzi unaotakiwa kufanywa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kuhusiana na mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliotendeka wakati wa mzozo baada ya uchaguzi.

Serikali ya Cote D'Ivoire inataka mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC kuchunguza tu matukio ambayo yametokea katika muda wa miezi sita iliyopita. Vyama vya kijamii vinataka mahakama hiyo ya kimataifa kuangalia ukiukaji wa haki za binadamu uliotokea nchini Cote D'Ivoire katika muda wa muongo mmoja uliopita, ili kuweza kupata maridhiano ya kweli nchini humo.

Mzozo wa hivi sasa haukuanza katika uchaguzi wa mwaka 2010, una mizizi yake kuanzia Septemba 2002 , wakati wa jaribio lililoshindwa la mapinduzi na kusababisha uasi wa kijeshi. Kwa mujibu wa Hokou ambaye ni rais wa muda wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake makuu mjini Abidjan , League for Human rights, ni muhimu kuwa wale waliohusika na uhalifu wa hali ya juu tangu mwaka 2002 watambuliwe , wafikishwe mahakamani na waadhibiwe. Iwapo tutazuwia kiwango cha uchunguzi, amesema, tunawatelekeza wale waliofariki wakati wa kipindi hicho.

Anaamini kuwa baada ya miaka mingi ya mzozo, nchi hiyo haiwezi kusonga mbele kuelekea kupata maridhiano ya kudumu na ya kweli iwapo itafanya sehemu tu ya maumivu , ambayo jamii imepitia.

Patrick N'Gouan, rais wa shirika lisilo la kiserikali la Societe Civile Ivoirienne , linakubaliana kuwa ICC inapaswa kuchangia katika kuleta maridhiano nchini Cote D'Ivoire na ni lazima iepuke hukumu ambazo zitaelemea upande mmoja. Bila hivyo ni hali ambayo itapanda mbegu za mzozo mwingine kama wa 2002.

lakini serikali ya Cote D'Ivoire haikubaliani na mawazo hayo. Sifikiri kuwa leo hii tutakuwa na kesi kwa ajili ya matukio ambayo yametokea miaka kadha iliyopita. Tunahitaji kuangalia zaidi matukio ya hivi karibuni na yale ya hivi sasa, amesema Bruno Kon, ambaye ni msemaji wa serikali.

Iwapo mtu anataka kurejea nyuma , kwa hiyo anapaswa kwanza kurejea katika matukio ya mwanzo kabisa. Na hilo ni suala gumu kufanyika, ameongeza. Hata hivyo Kon amefafanua kuwa watu ambao wameteseka na uhalifu ama kupoteza mali wanaweza kutumia mfumo wa sheria wa hapa nyumbani. Ili mradi sheria ya muda haijapita, mfumo wa sheria wa taifa unaweza kulishughulikia suala hilo. Kwa hiyo matukio ya zamani yataangalia kwa undani.

Mwanasheria wa mjini Abidjan Abraham Gadji anaona hali hiyo kuwa isiyowiana. Hii ina maana kuwa sheria za kimataifa zitawezeshwa kufuatilia watu waliofanya uhalifu katika mzozo wa hivi karibuni. Lakini katika matukio yaliyotukia karibu muongo mmoja , mtu anatakiwa kwenda katika mahakama za kitaifa. Hii inaonekana kuwa na hali ya kuzuwia na kuwapo kwa sheria ambayo haina usawa.

Anaamini kuwa kuweza kupata haki kwa makosa yote ya kihalifu yaliyotokea kati ya mwaka 2002 na 2010 kunahitaji uchaguzi ama mahakama ya ICC ama mahakama za Cote D'Ivoire kuweza kutoa hukumu. Huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na wale wanaohusika ni lazima watambuliwe. Gadji ametaja , miongoni mwa matukio hayo kuwa ni pamoja na mauaji katika vijiji vya Guitrozon na Petit Dukou ambapo yametokea mauaji ya watu zaidi ya 150 wakati wa maandamano ya upinzani mwezi March mwaka 2004, mauaji ambayo hayajapatiwa ufumbuzi ya rais wa zamani Robert Guy na waziri wa mambo ya ndani Boga Doudou, ambao wote waliuwawa wakati wa jaribio lililoshindwa la mapinduzi mwaka 2002, pamoja na mauaji na miili 57 iliyogunduliwa katika kaburi la pamoja katika eneo la Yopougon kaskazini mashariki ya mji mkuu Abidjan.

Mwandishi : Sekione Kitojo / IPS

Mhariri : Maryam Dodo Abdallah.