1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la kigaidi la Berlin na athari zake

Oumilkheir Hamidou
21 Desemba 2016

Mashambulio ya kigaidi ya Berlin na athari zake kisiasa na kijamii ndio mada iliyohanikiza magazetini hii leo. Mbali na mada hiyo, mkutano wa Moscow kuhusu hali nchini Syria pia umechambuliwa .

https://p.dw.com/p/2UeZf
Deutschland Breitscheidplatz nach dem Anschlag in Berlin
Picha: DW/F. Hofmann


Tunaanzia lakini Berlin na zilzala inayotokana na shambulio la kigaidi lililoangamiza maisha ya watu 12 na wengine wasiopungua 50 kujeruhiwa. Hakuna kutupiana lawama na wala hakuna kubadilisha mtindo wa maisha, wanakubaliana kwa sehemu kubwa wahariri wa magazeti ya Ujerumani . Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Hakuna chama chochote cha Ujerumani kinachostahiki kulaumiwa kwa shambulio la kigaidi lililotokea. Wakulaumiwa ni wale tu wanaotumia sababu za kinadharia au za kidini kutaka kuwapokonya watu haki za kuishi. Tunabidi tusimame kidete dhidi ya waasisi, waandalizi na wenye kuhubiri chuki.

Mtindo  huru wa maisha yetu tunabidi tuutetea kwa nguvu zote zilizoko. Jamii iliyo huru haistahiki kushindwa nguvu na waliopotoka na wasiokuwa na huruma. Ushenzi wa aina gani unaomfanya mtu kuendesha lori kubwa kama lile kati kati ya soko la X-Mas? Au kuficha mabomu ndani ya mikoba wanayobeba watoto mgongoni? Kamwe wanaofanya visa kama hivyo hawatoweza kuheshimiwa wala kupata nguvu.


Kinachowaudhi ni maadili yetu,ukarimu na mshikamano kati yetu

 

Gazeti la "Main Post" linashadidia pia umuhimu wa mshikamano miongoni mwa jamii ili kuwashinda nguvu magaidi. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Lengo kuu la magaidi sio kuuwa watu mpata mpatae na kuwajeruhi-kama ilivyobainika katika uwanja wa kanisa la Gedächniskirche. Wanataka kwa kufanya mashambulio yao ya kishenzi kuihujumu jamii nzima-kwa hivyo kila mmoja kati yetu. Kinachowaudhi ni maadili yetu, ukarimu wetu, uhuru, uvumilivu na mshikamano kati yetu. Yote hayo yanawachoma, yanawaudhi. Ndio maana tunabidi tusikate tamaa.Tusiachie ugaidi na matumizi ya nguvu kuamua kuhusu maisha yetu. Hata kama shambulio la wenye woga la mjini Berlin limetushtuwa, tusiachie likawa sababu ya kubadilisha mtindo huru wa maisha yetu. Kwasababu kwa namna hiyo, ugaidi ndio utakuwa umeshinda. Ni kweli kwamba maadili yetu ndiyo yaliyolengwa, lakini tusikubali yavurugwe.

 

Urusi,Iran na Uturuki kugawana keki ya Syria

 

Mada ya pili magazetini inahusu mkutano wa pande tatu ulioitishwa mjini Moscow kuzungumzia hali ya siku za mbele nchini Syria. "Maajabu yanatokea katika jukwaa la kisiasa: Katika kadhia ya Syria hivi sasa kumeibuka aina ya ajabu ya muungano kati ya Moscow, Teheran na Ankara-ushirikiano ambao miezi michache iliyopita ilikuwa shida kuufikiria na hasa upande wa serikali ya mjini Ankara. Rais Erdogan amegeuka  hivi sasa kuwa mshirika wa Assad. Zamani alikuwa rafiki, baadae akageuka adui mkubwa na sasa kama hajageuka tena kuwa rafiki, angalao amegeuka kuwa mshirika katika mchezo huu wa kuania madaraka na ushawishi. Kwa namna hiyo Assad anaweza kuendelea kuwepo madarakani. Sio kwa Syria nzima, lakini angalao kwa sehemu kubwa na muhimu ya nchi hiyo. Wanaomdhamini ni warusi na wairan. Waturuki wanaweza kutegemea kudhibiti sehemu ya kaskazini ili kuwazuwia wakurd. Kama ufumbuzi wa aina hiyo utaleta amani?Kuna wanaoshuku.

 

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga