1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHAMR El SHEIKH : Rice akutana na mwenzake wa Syria

4 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC4z

Kutokuwepo kwa mawasiliano ya ngazi ya juu ya kidiplomasia kati ya Marekani na Syria kwa miaka miwili kumemalizika hapo jana wakati Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice alipokutana na waziri mwenzake wa Syria.

Rice alizungumza na Walid al- Moalem pembezoni mwa mkutano wa kimataifa juu ya mustakbali wa Iraq katika mji wa Sharm el - Sheikh nchini Misri.Amesema kufuatia mazungumzo yake hayo kwamba ameitaka serikali ya Syria kulishughulikia tatizo la wapiganaji wa kigeni kuingia Iraq kwa kutokea Syria.Rice pia amesema hafuti uwezekano wa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki.

Wakati wa mazungumzo ya mkutano huo washiriki wameahidi kufuta madeni ya kigeni ya dola bilioni 30 kwa Iraq.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuisaidia Iraq.

Saudi Arabia inafuta asilimia 80 ya madeni yake kwa Iraq lakini imetaka kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kuwalinda Waislamu wa madhehebu ya Sunni walio wachache nchini humo.