1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHARM EL –SHEIKH : Mubarak akutana na Olmert

5 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdJ

Rais Hosni Mubarak wa Misri na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert hapo jana wamekuwa na mazungumzo ya kujaribu kufufuwa mchakato wa amani uliokwama wa Mashariki ya Kati lakini mkutano wao umeonyesha kutofautiana sana.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye mji wa kitalii wa Bahari ya Shamu waSharm el Sheikh Mubarak alianza kwa kukosowa kujiingiza kwa Israel katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah kulikopelekea kuuwawa kwa Wapalestina wanne na kujeruhi wengine 20 hapo jana.

Kiongozi huyo mkongwe wa Misri ameelezea kupinga kwake na kulaani operesheni za kijeshi za Israel huko Ramallah na harakati zozote zile nyengine ambazo zinaweza kukwamisha jitihada za kufikia amani ametowa wito kukomeshwa mara moja kwa umwagaji damu.

Mubarak amesema usalama wa Israel hautopatikana kwa nguvu za kijeshi bali kwa nia ya kweli ya kutaka amani.

Wakati Waziri Mkuu wa Israel Olmert akielezea masikitiko yake juu ya kupotea kwa maisha ya watu amesisitiza haja ya kujihami ambapo amesema Israel itachukuwa hatua zote kuzuwiya magaidi kuwadhuru raia wake.

Mkutano huo umeshindwa kutangaza mabadilishano yoyote yale ya wafungwa kati ya Israel na Wapalestina.