1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shauri la Obama kwa Urusi lichangie kurekebisha uhusiano ?

4 Machi 2009

Na je, komputa zitumike kupigia kura ?

https://p.dw.com/p/H5Nq

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo, yamegusia mada za nje na za ndani. Nje, ni juu ya shauri la Rais Obama kwa Urusi kuwa tayari kuacha kutega makombora ya Marekani huko ulaya ya Mashariki ikiwa Urusi nayo, itaishawishi Iran kuachana na mradi wake wa nuklia.

Ndani , ni kuhusu hukumu ya kupiga marufuku matumizi ya komputa kupigia kura kwa vile, matumizi ya komputa yatoa mwanya wa kufanya mizengwe katika uchaguzi.

Hukumu ya pili ni juu ya waziri mkuu Althaus wa mkoa wa Thuringen kwa kusababisha kifo katika ajali ya kumpiga dafurao mwanamke wakati wa mchezo wa barafuni wa (skii ) nchini Austria.

Gazeti la Bonn "GENERAL-ANZEIGER" laandika:

"Shauri la Rais Obama linaziwezesha pande zote mbili kuzika tofauti zao bila kuona haya; tofauti ambazo kwa miezi kadhaa sasa zimetia sumu uhusiano kati ya Washington na Moscow. Na kuna sababu za kutosha za kurejesha uhusiano mwema na Urusi"

Tukigeukia mada za ndani, gazeti la KOLNER STADT-ANZEIGER linazungumzia kuporomoka jana kwa jengo la kale la makumbusho mjini Cologne likiandika:

"Hakuna msiba uliozuka mjini Cologne mnamo mwongo uliopita uliowaathiri watu mno kama huu wa kuanguka Jumba hilo lenye dafutari za kihistoria. Bado si wazi i ni watu wangapi wamefariki au kujeruhiwa na kwa kadiri hakuna taarifa juu ya hayo, wasi wasi mkubwa unabaki.

Zaidi ni hasara kubwa katika hazina ya Jumba hilo. Hasara hiyo haiwezi kutathminiwa kwa hesabu au kwa masafa ya rafu za dafutari ziliomo. Kwani ni hazina ya ukumbusho wa mji wa Cologne.

Taarifa zilizoibuka kwamba maonyo mengi yametolewa kuhusu ufa ulioingia katika Jumba hilo, kunabainisha baruti za mripuko wa kisiasa. Ni nani alipuuza maonyo hayo? Wakuu wa jiji la Cologne wanapaswa kuchunguza na kujibu ili wasipoteze imani, imani ambayo kwa kutokea ajali hii tayari imepungua ."

Gazeti la LUBECKER NACHRICHTEN laichambua hukumu aliopitishiwa waziri mkuu Althaus wa jimbo la Thuringen. Laandika:

"Bw.Dieter Althaus kwa madhambi aliofanya ameteketeza maisha ya mwanadamu na ukumbusho wa kitendo hicho utasalia. Na huo ni mzigo mzito mabegani mwake na iwapo katika hali hiyo aweza kusalia na wadhifa wake mkuu, ni jambo linalostahiki haraka kuamuliwa."

Likitukamlishia mada yetu ya mwisho: iwapo mitambo ya komputa yafaa kutumika katika upigaji kura, hukumu ya Mahkama Kuu ya Ujerumani inasema la,haifai.

Gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten likiichambua hukumu hiyo laandika:

"Mahkama kuu ya Katiba kwa hukumu yake ya kuzuwia matumizi ya komputa katika kupigia kura kwenye uchaguzi, imetoa mchango wa kusifiwa sana katika kuleta hali ya uwazi na maamuzi ya kisiasa. Sauti za wapigakura lazima zithaminiwe vile walivyoamua na sio vyengine...."

SUDWEST-PRESSE linatuzindua:

"Madaraka ya kutawala yanahitaji ridhaa ya wapiga kura.Katika demokrasia, madaraka hayo yanatokana na uchaguzi. Endapo matokeo ya upigaji kura huo yatakuwa na shaka shaka, basi imani kwa dola inapotea."