1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheikh Mohammed aungama

15 Machi 2007

Mpikajungu la mashambulio ya Septemba 11,2001 asemekana aungama madhambi yake.

https://p.dw.com/p/CHI5
Picha: AP

Mtuhumiwa mkuu na mpikajungu wa hujuma za Septemba 11,2001 huko Washington na New York, Khalid Sheikh Mohammed-raia wa Pakistan,anaripotiwa eti ameungama kupanga njama hizo kuanzia mwanzo hadi mwisho.Sheikh Mohammed anasemekana kutoa taarifa hiyo katika kikao cha faragha cha kumhoji katika gereza la guantanamo.Katika taarifa yake ,Sheikh Mohammed asemekana kuungama kwamba alikuwa dhamana wa opresheni nzima pamoja na hujuma nyengine zilizofungamanishwa na mtandao wa Al Kaida.

Kwa jumla, Mohammed amesema aliandaa njama 29 pamoja na ile ya jaribio la mpachika-bomu kwenye viatu-Richard Reid (shoe-momber) ili kuripua ndege ya abiria na hujuma ya mabomu bali,Indonesia.

Itakumbukwa Septemba 6 mwaka jana Khalid Sheikh Mohammed alikokotwa hadi kambi ya CIA ya gereza la Guantanamo,kisiwani Kuba.

Katika hotuba yake maarufu ambamo kwa mara ya kwanza alifichua kuwapo gereza la Guantanamo,rais George Bush alimtaja KSM-yaani Khalid Sheikh mohammed:

“KSM amehojiwa na CIA kwa kutumia utaratibu maalumu na yeye amefichua habari-ambazo zimeongoza kuzima hujuma zaidi zilizopangwa nchini Marekani.KSM alitupa pia taarifa za njama nyengine za kuwahilikisha wamarekani wasio na hatia yoyote.”

Kwa kufikishwa Guantanamo kwa Khalid Sheikh Mohammed na wenzake 13 wanaotiliwa shaka ugaidi,aliesema rais Bush kwamba gereza hilo la CIA sasa limefungwa.

Gereza hilo hivi sasa wafungwa wake wapya wanaorodheshwa katika daraja mbali mbali:

Daraja hizo zaitwa CSERT.Tume ya kijeshi ya watu 3 inaamua iwapo mfungwa aorodheshwe kama ni-“Enemy combatants”-yaani mpiganyaji adui au bado ni hatari sana na wana habari muhimu za siri.Tume hii ya kijeshi si mahkama na wafungwa hawalazimiki kufika mbele yake.

Kwa muujibu wa taarifa za jioni zilizochapishwa na wizara ya ulinzi ya Marekani –Pentagon- Khalid Sheikh Mohammed, alifika mbele ya tume hiyo Machi 10 na akaungama mambo kadhaa.Alisema ni yeye aliepika jungu la hujuma ya kwanza katika Jengo la Biashara la World Trade Center huko New York, 1993 hata lile la pili la Septemba 11,2001.

Amenukuliwa Sheikh Mohammed kusema hivi:

“Ni dhamana tangu A-Z-tangu mwanzo hadi mwisho wa hujuma hizo.”

Taarifa alizoungama mpakistani huyo zinathibitisha kile alichosema rais George Bush Septemba mwaka jana .Katika wimbi la hujuma ya pili, ilipangwa kutumia ndege za abiria kuhujumu Library Tower mjini Los Angeles,Sears Tower mjini Chicago,Plaza bank mjini Seattle pamoja na Empire State Building mjini New York.

Sheikh Mohammed aliekua nambari 2 wa Osama Bin Laden katika mtandao wa Al Kaida, anasemekana muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni na maajenti wa shirika la ujasusi la Marekani CIA mwaka 2003,aliteswa.Hakuna mashahidi huru kuwa Khalid Sheikh Mohamme ameungama hayo anayosemekana kuugama huko Guantanamo.

Kinyume na desturi, wakati taarifa hizi zinatolewa hapo jana, waandishi habari hawakualikwa.Sababu iliotolewa –kuficha siri za taifa.Taarifa iliotolewa sehemu nyingi ya vifungu vyake ilipigwa michoro isisomeke.

Inafahamika kwamba,Khalid Sheikh Mohammed alitaka kuhetimisha taarifa yake kwa kusema kwamba

anahuzunishwa kuona binadamu wameuwawa,lakini kifo, ndio lugha ya vita na vita kama sehemu ya maisha kamwe havimaliziki.