1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria inayobishwa imebatilishwa Ufaransa

29 Februari 2012

Baraza la katiba nchini Ufaransa limebatilisha sheria inayomuadhibu yeyote anaekanusha mauwaji ya halaiki ya waarmenia ya mwaka 1915.Rais Sarkozy ametoa mwito wa kutungwa mswaada mwengine wa sheria.

https://p.dw.com/p/14BpS
Bendera ya Ufaransa na Uturuki zapeperushwa baada ya baraza la katiba kubatilisha sheria dhidi ya wanaobisha kama kulifanyika mauwaji ya halaiki ya waarmeniaPicha: picture-alliance/dpa

Baraza la katiba linahoji "kwa kuwakandamiza wale wanaobisha kama mauwaji hayo yamefanyika na kuhalalisha kisheria visa ambavyo wenyewe walivitambua kuwa ni vya uhalifu, ni kinyume na uhuru wa mtu kutoa maoni yake na uhuru wa mawasiliano."

Wanachama wa baraza la katiba wamekitumia kifungu nambari 11 cha mwaka 1789 kinachozungumzia kuhusu haki za binaadam ,kinachosema "uhuru wa kubadilishana fikra na mawazo ni mojawapo wa haki adimu za binaadam."

Uturuki hapo hapo ikaelezea kuridhika kwake na uamuzi huo wa baraza la katiba la Ufaransa.Msemaji wa ubalozi wa Uturuki mjini Paris Engin Solakoglu amesema uamuzi huo unatoa matumaini mema ya kuimarishwa uhusiano kati ya Ufaransa na Uturuki.

Uamuzi huo umeepusha pasitokee "mzozo mkubwa " kati ya nchi hizi mbili,amesema kwa upande wake naibu waziri mkuu wa Uturuki Bülent Arinc.

"Baraza la katiba limetoa uamuzi wa haki,ambao haukushawishiwa na hisia za kisiasa"amesema bwana Arinc kupitia Twitter.

Sarkozy erklärt Präsidentschaftskandidatur im französischen Frankreich
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: REUTERS/TF1

Sheria hiyo iliyoidhinishwa na bunge la Ufaransa january 23 mwaka huu,ilikuwa ikiungwa mkono na rais Nicolas Sarkozy.Hapo hapo kiongozi huyo wa Ufaransa anaegombea mhula wa pili madarakani,ameitaka serikali yake itunge mswaada mwengine,kwa kuzingatia uamuzi wa baraza la katiba.

Taarifa kutoka kasri la rais huko Elysée inasema tunanukuu:"Rais anazingatia uamuzi uliopitishwa na anatambua masikitiko na huzuni za wale waliokaribisha kwa mikono miwili sheria hiyo ilipopitishwa-sheria iliyokuwa imelengwa kuwahifadhi dhidi ya wale wanaokanusha mauwaji hayo ya halaiki.

Mswaada wa sheria dhihdi ya kukanusha mauwaji ya waarmenia ulifikishwa bungeni December 22 mwaka jana na kuzusha ghadhabu za waturuki,huku waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan akifika hadi ya kusema mswaada huo unatoa picha ya kuzidi chuki dhidi ya dini ya kiislam na ubaguzi barani Ulaya."

Baada ya mswaada huo ulipopigiwa kura,Uturuki,mwanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO ikasitisha ushirikiano wa kisiasa na kijeshi pamoja na Ufaransa.Serikali ya Ankara iliahidi kuchukua hatua kali zaidi pindi sheria hiyo ingeidhinishwa.

Rais Nicolas Sarkozy amekuwa tangu mwanzo akijaribu kutuliza mvutano huo katika wakati ambapo mswaada wa sheria ulikuwa ukibishwa hata miongoni mwa wanachama wa serikali yake.

Armenien Frankreich Genozid Völkermord Vertreibung Denkmal in Eriwan Nicolas Sarkozy und Serge Sarkisian
Rais Nicolas Sarkozy (kushoto) na rais Serge Sarkisian wa Armenia wakizuru kumbusho la mauwaji ya halaiki ya waarmenia huko YerevanPicha: AP

Uamuzi wa baraza la katiba umekosolewa na baraza linalosimamia mashirika ya watu wenye asili ya Armenia nchini Ufaransa.LInadai baraza la katiba limesalim amri mbele ya shinikizo la Uturuki.

Uturuki daima imekuwa ikikataa kutumiwa neno mauwaji ya halaiki.Kwa mujibu wa wana historia waarmenia milioni moja na nusu,waliuliwa huko Anatolia kati ya mwaka 1915 na 1917.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/Afp

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed