1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ya hali ya hatari ya 2015 yafikia mwisho wake leo

Zainab Aziz
1 Novemba 2017

Nchini Ufaransa sheria ya hali ya hatari iliyowekwa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya mjini Paris mnamo mwezi Novemba mwaka 2015, imefikia mwisho wake leo hii. Lakini sheria mpya ya ugaidi imeanzishwa.

https://p.dw.com/p/2mqN2
Frankreich Paris - Polizeiaufgebot am Eifelturm
Picha: Getty Images/AFP/K. Tribouillard

Hali hiyo ya hatari iliwekwa nchini Ufaransa, baada ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislam kuwaua watu wapatao 130 mjini Paris mnamo ,wezi Novemba mwaka 2015. 

Hali hiyo ya dharura iliongezewa muda kwa mara ya sita pale ilipopigiwa kura bungeni mnamo mwezi Julai na leo hii tarehe moja mwezi Novemba ndio inafikia mwisho wake hivyo basi kupisha sheria kadhaa kali zilizoidhinishwa na rais Emmanuel Macron siku ya Jumatatu. 

Rais Macron aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter  "Ahadi imetimia hali ya hatari imefikia mwisho leo tarehe 1 mwezi Novemba ni wakati sasa wa kuimarisha usalama wa wananchi wetu''.

Frankreich Macron will Einwanderungspolitik verschärfen
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/P. Wojazer

Hatua hizo za kiusalama zimekuwepo nchini Ufaransa tangu Novemba mwaka 2015. Sheria, zilizoidhinishwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni mojawapo kati ya ahadi kuu za kampeni ya Macron.

Kiongozi huyo amesema chini ya sheria mpya, polisi watakuwa na nguvu zaidi ya kufanya msako na kuwakamata washukiwa bila idhini ya mahakama na vilevile polisi watakuwa na uwezo wa kuzuia harakati na mikusanyiko ya watu. 

Licha ya Ufaransa kukabiliwa na hatari ya kutokea mashambulio ya kigaidi, sheria hiyo mpya imekosolewa na wakosoaji wa ndani wa serikali ya Ufaransa, ambao wanasema sheria hiyo itadhoofisha maadili ya nchi hiyo na uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya kukusanyika.

Sheria hiyo mpya pia imekosolewa na mkuu wa ofisi inayochunguza malalamiko ya wananchi ya nchini Ufaransa Jacques Toubon, ambaye anasema kwamba kuuwekea vikwazo uhuru wa watu binafsi kwa jutumia misingi ya tuhuma ni kukiuka moja kwa moja kanuni za msingi za sheria ya jinai.

Baraza la seneti limerekebisha rasimu ya awali ya serikali ili kuhakikisha kuwa sheria hiyo itafikia ukomo wake mwishoni mwa mwaka 2020.

Vikosi vya usalama pia vitakuwa na uwezo wa kumsimamisha mtu yeyote na kuangalia utambulisho wa mtu huyo kwa umbali wa kilomita 10 kutokea kwenye bandari kuu au viwanja nya ndege vya kimataifa.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga