1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ya hali ya hatari yaondolewa.

16 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CcDt

Islamabad. Rais wa Pakistan Pervez Musharaff ameondoa sheria ya hali ya hatari aliyoiweka nchini mwake mapema mwezi wa Novemba. Musharraf ametetea sheria hiyo ya hali ya hatari akisema kuwa ilikuwa muhimu ili kuweza kupambana na ghasia zilizokuwa zinazidi kuongezeka na kushughulikia idara ya sheria ambayo ilikuwa inadhoofisha serikali.

Uchaguzi unatarajiwa kufanyika nchini humo mwezi ujao wa Januari , na mawaziri wawili wa zamani Nawaz Sharif na Benazir Bhuto , ambaye amerejea hivi karibuni nchini humo kutoka kuishi uhamishoni, wanapanga kugombea.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuondolewa kwa sheria hiyo ya hali ya hatari bibi Bhuto amesema kuwa kuondolewa kwa sheria ya hali ya hatari ni hatua muhimu.

Kuondolewa kwa sheria ya hali ya hatari ni hatua muhimu katika kipindi hiki cha mpito kutoka udikteta kuelekea demokrasia. Lakini athari zake katika mpango mpya wa katiba, kundi la wanasheria katika chama chetu Peoples Party, linaliangalia suala hilo kwa makini, na baada ya kulichunguza tutakuwa katika nafasi ya kutoa jibu letu. Lakini hadi sasa tunaweza kusema kuwa kuondolewa kwa sheria ya hali ya hatari ni hatua muhimu. Hata hivyo kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kufanywa na ni masuala ya demokrasia.

Wakati huo huo , shambulio la kujitoa muhanga dhidi ya kituo cha jeshi kaskazini magharibi ya Pakistan limesababisha vifo vya watu wapatao watano.