1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo dhidi ya Hamas laongezeka

Mohamed Dahman18 Oktoba 2008

Misri hivi karibuni imefunguwa tena mpaka wake na Ukanda wa Gaza kwa usafiri wa watu wachache kabla ya kuanza kwa mkutano unaokuja wa usuluhishi wa Wapalestina uliopangwa kufanyika mjini Cairo mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/FcOW
Mahasimu wa Kipalestina Rais Mahmoud Abbas kushoto wa kundi la Fatah na kiongozi wa Hamas Khaled Mashaal, wa pili kulia na aliekuwa Waziri Mkuu wa Wapalestina Ismail Haniyeh, kulia , pia wa kundi la Hamas wakati walipokutana Mecca Saudi Arabia mwezi wa Februari mwaka 2007 kwa mazungumzo ya kushirikiana madaraka.Picha: AP

Lakini baadhi ya wachambuzi wa kujitegemea wanasema Misri imekuwa tu ikiutumia mpaka huo kama njia ya kulishinikiza kundi la upinzani la Hamas kukubali mapendekezo yake ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Wapalestina.

Hatem al - Bulk ameliambia shirika la habari la IPS kwamba serikali ya Misri inatumia kadi hiyo ya mpaka kuishurutisha Hamas kukubali masharti ya usuluhishi na kundi la Fatah.

Anasema wakati Hamas inapokuli kuridhia masharti yake ya kushiriki mkutano huo Misri hufunguwa mpaka wake huo na wakati Hamas inapokaidi huufunga mpaka huo.

Kwa siku tatu mwezi uliopita Misri ilifunguwa mpaka huo uliofungwa tokea Hamas ilipochukuwa madaraka katika Ukanda wa Gaza mwaka jana kwa usafiri wa watu wachache. Uamuzi huo umekuja licha ya madai kutoka kwa maafisa wa Israel kwamba magaidi wa Kipalestina wanaweza kutumia fursa hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya Waisrael walioko mapumzikoni katika Ghuba ya Sinai nchini Misri.

Kuanzia Septembe 20 hadi 22 mpaka wa Rafah ulifunguliwa kwa takriban wanafunzi 2,500 wa Kipalestina, wagonjwa wanaohitaji matibabu na mahujaji waliokuwa wakielekea Saudi Arabia.

Hata hivyo kutokana na pingamizi ya Israel al-Bulk anasema siku iliyofuatia urasimu uliongezeka na wanafunzi kadhaa walinyimwa kibali cha kuvuka mpaka huo.

Kufunguliwa huko kwa mpaka kwa watu wachache kumekuja wakati Misri ikiongeza juhudi zake za kufikiwa kwa makubaliano ya usuluhishi wa kitaifa kati ya Hamas na Fatah kundi la serikali ya Mamlaka ya Wapalestina inayoungwa mkono na Marekani ya Rais Mahmoud Abbas yenye makao yake huko Ukingo wa Magharibi.Tokea Hamas inyakuwe udhibiti wa Gaza kutoka Mamlaka ya Wapalestina katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya kushtukiza mwaka jana makundi hayo mawili yamekuwa yakiendeleza uhasimu mkubwa kwa kamata kamata ya watu ovyo na mapigano ya hapa na pale ambayo yamekuja kuleta taathira mbaya kwa mapambano ya Wapalestina ya kuwania taifa lao.

Wakati Hamas ikifuata sera ya upinzani dhidi ya kukaliwa kwa mabavu kwa ardhi yao na Israel Fatah inashikilia mkakati wa mazungumzo na taifa hilo la Kiyahudi licha ya kushindwa hadi hivi sasa kufanikisha manufaa yoyote yale kwa upande wa Wapalestina.

Katika wiki za hivi karibuni maafisa wa Misri wamekuwa na mazungumzo tafauti mjini Cairo na makundi tafauti ya Wapalestina yakiwemo ya Hamas na Fatah kwa matumaini ya kufikia makubaliano kabambe ya mazungumzo yanayotarajiwa kusainiwa na makundi yote katika mkutano mkubwa wa usuluhishi mjini Cairo mapema mwezi ujao.Misri inataraji makubaliano hayo hatimae yatapelekea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Wapalestina.

Sambamba na makubaliano ya Wapalestina juu ya masharti ya serikali ya umoja wa kitaifa pendekezo la Misri pia linatowa wito wa kuwepo kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Hamas na Israel na pia kuitaka Hamas iache udhibiti mkubwa kupindukia wa Ukanda wa Gaza na kwa Israel kufunguwa kwa kudumu kivuko cha mpaka wa Gaza kwa usafiri wa binaadamu na vitu.

Iwapo mazungumzio hayo hayatokwamishwa na mabishano ya kisiasa yatawakilisha mkutano wa kwanza rasmi kati ya mahasimu hao mawili tokea Hamas inyakue Ukanda wa Gaza katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana baada ya kushinda uchaguzi katika ukanda huo hapo mwaka 2006.