1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo lazidi kumtaka Olmert ajiuzulu

Charles Mwebeya1 Mei 2007

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amekumbwa na shinikizo kubwa la kumtaka ajiuzulu, baada ya kutolewa ripoti ya uchunguzi wa vita ya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Lebanon.Tayari Waziri mmoja katika serikali ya Bwana Olmert amejiuzulu hii leo.

https://p.dw.com/p/CHF7

Shinikizo la kumtaka Bwana Olmert kuachia ngazi limeshika kasi zaidi katika chama chake cha Kadima, ambapo baadhi ya wanachama wamenukuliwa wakisema , Olmert hana chaguo jingine zaidi ya kuachia ngazi.

Vyombo vya habari nchini humo pia vimetabiri kujiuzulu kwa Waziri Mkuu huyo.

Magazeti mbalimbali nchini humo yamesema kutokana na kushindwa kwa vita dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon, Bwana Olmert amepoteza imani miongoni mwa wananchi .

Akizungumza kwa njia ya Televisheni, Bwana Olmert alikiri kuwapo kwa makosa kadhaa wakati jeshi lilipovuka mpaka na kuingia nchini Lebanon kwa nia ya kuwaokoa wanajeshi wake wawili, wanaoshikiliwa na kundi la Hezbollah.

Lakini pamoja na kukiri makosa hayo, Bwana Olmert alisema hayupo tayari kujiuzulu.

Katika vita hiyo ya siku 34, raia zaidi ya 1000 wa Lebanon walipoteza maisha , sambamba na wanajeshi 160 wa Israel ,ilhali wanajeshi wawili wa nchi hiyo wakiwa bado wanashikiliwa na Hezbollah hadi hivi sasa.

Ripoti ya tume maalum ya uchunguzi wa vita hiyo ya mwaka jana, ilimlaumu Bwana Olmert kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kufanya maamuzi ya pupa .

Ripoti hiyo ilifanya uchunguzi wake kwa muda wa miezi sita chini ya Jaji Eliahu Winograd

Ripoti hiyo vile vile haikuwaweka kando Waziri wa Ulinzi Amir Peretz na Mkuu wa zamani wa majeshi Dan Halutz.

Lakini katika kile kinachoonekana kuanza kumong’onyoka kwa serikali ya Muungano ya Bwana Olmert, Waziri asiyekuwa na Wizara maalum kutoka chama cha Labour, Eitan Cabel , ametangaza kujiuzulu kutoka serikali ya muungano.

Akitangaza uamuzi wake Bwana Cabel amesema hawezi kufanya kazi katika serikali inayoongozwa na Olmert, kutokana na makosa yaliyofanyika katika vita hiyo.

Chama anachotoka Bwana Cabel cha Labour , kiliungana na chama cha Kadima na kuunda serikali.

Mpaka hivi sasa bado haijawekwa wazi endapo mawaziri wengine kutoka chama cha Labour watafuata nyayo za Bwana Cabel .

Fukuto la kumtaka Olmert kujiuzulu limejikita miongoni mwa wananchi wa kawaida, ilhali maandamano makubwa yakiandaliwa mjini Tel Aviv, keshokutwa .

Pamoja na shinikizo hilo kutoka ndani , Habari zinasema Waziri Mkuu huyo anaungwa mkono na Marekani kuendelea na wadhifa huo.

Msemaji wa Ikulu ya Washington , amesema Rais Bush anamuona Olmert kama mtu muhimu, katika muafaka wa amani ya mashariki ya kati.