1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo za kumtaka Musharraf kuondoa hali ya hatari Pakistan zaendelea

Jane Nyingi8 Novemba 2007

Marekani imepongeza hatua ya rais Pervez Musharraf wa Pakistan kutangaza kuwa uchaguzi mkuu utafanyika kabla ya tarehe 15 mwezi februari mwaka ujao. Rais George Bush wa marekani amejiunga na viongozi wengine wa mataifa ya magharibi wanaotaka uchaguzi huo ufanywa wakati ufaao na pia kondolewa kwa hali ya hatari iliyotangazwa na rais Musharraf.

https://p.dw.com/p/C775
Rais wa Pakistan Pervez Musharraf
Rais wa Pakistan Pervez MusharrafPicha: AP

Tangazo hilo la Musharraf limepuuziliwa mbali na aliyekuwa waziri mkuu Benazir Bhutto na kusema ataendelea na mipango yake ya kuongoza maandamano ya maelfu ya wafuasi wake katika mji wa Rawalpindi karibu na Islamabad hapo kesho.Rais Musharraf ambaye alipongezwa na marekani kwa ushirikiano wake katika vita dhidi ya ugaidi na kukabiliana na wanamgambo wa kitaliban amesema amejitolea kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika na uongozi wa kiraia kurejeshwa.Ujerumani ni miongoni mwa mataifa ambayo yametoa sauti zao yakimtaka Musharraf kuondoa hali hiyo ya hatari nchini Pakistan.

Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali kilitangaza kama taarifa ya ghafla tangazo la rais Musharraf kwa mara nyingine kuwa atangatuka madarakani kama mkuu wa majeshi kabla ya kuapishwa kuongoza kwa muhula wa pili. Hata hivyo hakutangaza ni tarehe atakayofanya hivyo.

Musharraf ambaye aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya mwaka 1999 hawezi kuapishwa hadi mahakama kuu ihalalishe ushindi wake katika uchaguzi wa urais tarehe 6 mwezi october ambao ulimuidhinisha kubakia madarakani kwa miaka mingine mitano.Wengi katika serikali wanahisi kuwa aumuzi wa mahakama huenda ukawa dhidi yake na ndiposa akaamua kutangaza hali ya hatari siku ya jumamosi. Rais Musharraf alisema alichukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu na kuingiliwa kwa shughuli za mahakama.

Tangazo hilo la siku ya kufanyika kwa uchaguzi lilitolewa saa kadhaa baada ya mkuu wa sheria nchini Pakistan kuwaambia wanahabari wa shirika la kimataifa la AFP kuwa hali hiyo ya hatari itaondolewa katika muda wa mwezi mmoja ua miezi miwili ijayo.

Bhutto alisema tangazo hilo la rais Musharraf niliwakufumba macho,akiongeza kuwa anapaswa kujizulu kama mkuu wa majeshi wiki ijayo.Bali na maandamano hayo ya hapo kesho bi Bhutto amesema ataongoza maandamano mengine kutoka Lahore hadi Islambad tarehe 13 mwezi huu."Tunataka siku kamili ya kufanywa kwa uchaguzi huo mkuu na siku kamili atakapongatuka madarakani kama mkuu wa majeshi" Bhutto amewambia wanahabari.

Taarifa nyingine ni kuwa Wanasiasa watatu na mwanaharakati hivi leo wameshtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na hutoba zao za kuipinga serikali mjini Karachi nchini Pakistan. Wanne hao ndio wa kwanza kukabiliwa na shtaka hilo ambalo hukumu yake ni kifo, tangu rais Musharraf kutangaza hali ya hatari nchini humo siku ya jumamosi.