1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo zaidi la kimataifa lamtaka Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe an'gatuke

Mohamed Dahman6 Desemba 2008

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema leo hii kwamba mataiafa makubwa duniani lazima yashirikiane kumueleza Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kwamba aliyoyafanya yanatosha.

https://p.dw.com/p/GAdi
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.Picha: AP

Brown anasema hayo wakati kipindupindu nchini humo kikiwa kimeuwa takriban watu 600.

Brown amesema mgogoro nchini Zimbabwe sasa umekuwa wa kimataifa na kuongeza kusema kwamba anataraji Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kwa dharura kujadili hali hiyo.Amesema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake ya Downing Street kwamba mgogoro huo umekuwa wa kimataifa kwa sababu ugonjwa huo umevuka mipaka,mfumo wa serikali umesambaratika na hakuna serikali yenye uwezo au kuwa tayari kuwalinda wananchi wake.

Kauli yake hiyo inakuja wakati shinikizo la kimataifa dhidi ya Mugabe likiongezeka.Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Miliband ameita serikali ya Zimbawe kuwa ni utawala wa kihuni wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen amesema wakati umepindukia kwa Mugabe kun'gatuka.

Rice amesema wakati umepindukia kwa Mugabe kuondoka na anafikiri jambo hilo hivi sasa liko dhahiri na kwamba hivi sasa wanashuhudia sio tu athari za kisiasa na kiuchumi kwa wananchi wa Zimbabwe bali taathira hiyo imekuwa ya kibinaadamu kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini ametowa wito kwa Mugabe kujiuzulu au ashtakiwe na mahkama ya jinai ya kimataifa mjini The Hague Uholanzi kwa kuwakandamiza wananchi wake.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Uholanzi Tutu pia amesema itakuwa halali kumuondowa Mugabe kwa kutumia nguvu.