1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la FAO lasema bei ya nafaka imepanda mara dufu duniani

Kalyango Siraj11 Aprili 2008

Kupanda kwa bei ya nafaka kumesababisha ghasia katika baadhi ya nchi

https://p.dw.com/p/DgLG
Askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani Haiti akirusha gesi ya kutoa machozi kwa waandamanaji katika mji mkuu wa Port-au-Prince, Tuesday, April, 8, 2008. Walikuwa wanapinga kupanda kwa bei ya chakulaPicha: AP

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kupanda kwa bei ya vyakula duniani kwa weza kuendelea na hilo kutishia mamiliioni ya watu duniani wanaoishi kwa kutumia kipato cha dola moja kwa siku.

Hali hiyo imo katika ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia kilimo na chakula la FAO lilio na makao yake makuu mjini Roma nchini Italy.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa leo Ijumaa inasema kuwa bei za vyakula muhimu kama vile mkate,mchele, maziwa,mafuta ya kupikia pamoja na vyakula vingine muhimu imepanda mara dufu katika kipindi cha miezi kadha iliopita katika mataifa mengi yanayonukia duniani.

Ripoti inasema kuwa bei za nafaka zimepanda kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji,uhaba wa kuyatoa pamoja na vizuizi vipya kuhusu uagizaji.

Ingawa katika eneo la Afrika Mashariki hakujatokea maandamano pamoja na ghasia lakini kwingineko yametokea.Mfano katika kisiwa cha Haiti ghasia zilizuka wakati wananchi wakipinga uhaba wa chakula .Licha ya kiongozi wao kuwahimiza kubaki watulivu wao waliandamana na kuzusha ghasia.

Shirika la chakula na kilimo duniani,FAO,limeonya kuwa uhaba pamoja na kuongezeka kwa bei ya vyakula kutaongezeka na wakati fulani unaweza ukasababisha ghasia.

Hali ya kuendelea kupanda kwa bei ya vyakula pia iligusiwa katika mkutano wa kwanza kati ya mataifa ya kiafrika na India uliokuwa mjini Delhi,ambapo mataifa ya kiafrika yakishirikiana na India yaliapa kuzidisha juhudi za usalama wa chakula na pia kuzihimiza nchi za magharibi kupiga moyo konde kuhusu hatua yao ya kutaka kubadilisha shehena kubwa ya chakula walio nayo kuitumia katika njia zingine za kutengeneza nishati.

Mkutano wa India umeendelea kusema kuwa hatua hiyo ya mataifa tajiri imechangia uhaba wa chakula na hivyo kusababisha bei yake kupanda hasa katika mataifa yanayoendelea.

Hata hivyo ripoti ya FAO hiyo imesema kuwa hali inaweza ikawa borakutokana na uwezekano wa kupanda kwa uzalishaji wa nafaka duniani unatarajiwa kuongezeka mwaka huu kwa kiwango cha zaidi ya 2.6 asili mia.Uzalishaji wa mwaka huu wa nafaka unategemewa kuwa tani zaidi ya 2 .7 millioni.