1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la IAEA limeitaka Iran kushirikiana haraka

Saleh Mwanamilongo
15 Juni 2020

Kiongozi wa shirika la IAEA ,Jumatatu ameiomba kwa mara nyingine tena Iran kushirikiana haraka na kikamilifu ilikuwaruhusu wachunguzi wake kutembelea maeneo mawili ambayo yanaaminika Iran ilirutubisha madini ya Uranium.

https://p.dw.com/p/3dnmH
Rafael Grossi ,mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya nyuklia IAEA.
Rafael Grossi ,mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya nyuklia IAEA.Picha: picture-alliance/Photoshot

Kiongozi wa shirika la Umoja wa mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Mariano Grossi, Jumatatu ameiomba kwa mara nyingine tena Iran kushirikiana haraka na kikamilifu ilikuwaruhusu wachunguzi wake kutembelea maeneo mawili ambayo yanaaminika Iran ilirutubisha madini ya Uranium.

Mwito huo wa Grossi kwa Iran ulitolewa kufuatia mkutano kwa njia ya vidio mjini Vienna wa baraza la magavana wa shirika la IAEA.

''Tunatakiwa kushirikiana na hilo ni moja wapo ya mazungumzo yangu na viongozi wa ngazi ya juu wa Iran. Nimesikitishwa kuona kwamba hadi sasa hakujakuweko na maelewano na nitafanya juhudi ziwezekanavyo ili kufikia maelewano'. Ushirikiano ni muhimu. Tunatakiwa kufanya kazi pamoja ili kuweko na ufafanuzi unaotarajiwa'',alisema Grossi.

Mwezi Januari, Iran ilikataa uchunguzi kwenye maeneo mawili ambayo shirika la IAEA lilitaka kuyafanyia uchunguzi. Maeneo hayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na shughuli za urutubishaji wa madini ya uranium za hivi sasa, lakini yanahusika na miradi ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kijeshi ya mwaka 2000.

Kukataa huko kunadhoohofisha uwezo wa shirika la IAEA wa kutoa taarifa za kuaminika za kutokuweko na shughuli na vifaa vya nyuklia ambavyo havikutolewa ufafanuzi na serikali ya Iran, aliongeza kusema Rafael Grossi mbele wa wajumbe wa IAEA ambao wanashiriki kwenye mkutano wa kila baada ya miezi mitatu.

Iran yatishia kujiondoa kwenye mkataba wa 2015

Mkutano wa magavana wa shirika la IAEA, mjini Vienna Machi 10 ,2020
Mkutano wa magavana wa shirika la IAEA,mjini Vienna Machi 10 ,2020Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/IAEA/D. Calma

Utawala wa Iran umelezea kwamba haulazimiki tena kutoa taarifa kuhusu shughuli zake za kinyuklia zilizofanyika kabla ya mkataba wa 2015.

Mapema mwezi Machi,utawala wa Tehran ulililaumu shirika la IAEA kutowa taarifa hiyo kufuatia shinikizo la Israel na Marekani. Kuangaziwa upya kwa mipango ya zamani ya kinyukliya ya Iran kunaweza kuzusha mivutano mipya.

Kuhusu mipango yake ya kisasa, Iran ina ushirikiano wa wazi na wachunguzi wa shirika la umoja wa mataifa ambao wamepewa nafasi ya kutembelea maeneo yote muhimu.

Toka kujiondoa kwa Marekani kwenye mkataba kuhusu mpangowa nyuklia wa Iran mwaka 2018  na kuiwekea vikwazo nchi hiyo, Iran inajaribu kutoheshimu vipengee kadhaa vya mkataba huo ili kujikwamua kiuchumi.

Hatua ya hivi karibuni ya kutouheshimu mkataba huo, ni wakati Iran ilipotangaza kwamba itakiuka mkataba wa nyuklia wa 2015 na kuvuka viwango vya urutubishaji madini ya uranium endapo jumuiya ya kimataifa itaiwekea nchi hiyo vikwazo vipya vya silaha.

Ripoti ya shirika la IAEA ya mapema mwezi huu inaelezea kwamba Iran iliendelea kurutubisha madini yake ya uranium kwa kiwango cha juu ya kikomo kilichokubalika kwenye makubaliano ya mwaka 2015.

 

Vyanzo : DPA/ APE/AFPF