1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli ya kubadilishana wafungwa yaanza leo

Mwadzaya, Thelma16 Julai 2008

Wafungwa watano wa Lebanon wamehamishwa kutoka jela moja ya Israel na kusafirishwa hadi eneo la mpakani katika hatua iliyoridhiwa ya kubadilishana wafungwa.Maiti za wanajeshi wawili wa Israel nazo pia zimo msafarani

https://p.dw.com/p/EdEK
Karnit Goldwasser,mkewe Ehud Goldwasser mmoja ya wafungwa wa IsraelPicha: AP

Kundi hilo la wafungwa linajumuisha mpiganaji mmoja aliyeshtakiwa kwa kuhusika na vitendo katili katika historia ya Israel.


Baraza la mawaziri la Israel liliidhinisha hapo jana hatua ya kumuachia huru Samir Kuntar.Kwa upande wake inataraji kurejeshewa maiti za wanajeshi wawili Eldad
Regev and Ehud Goldwasser ambao walikuwa hawajulikani waliko tangu kutekwa na kundi la Hezbollah miaka miwili ilyiopita.Isaac Herzog ni Waziri wa masuala ya Jamii nchini Israel na ameelezea msimamo wa serikali yake.

''Serikali ya Israel imefanya uamuzi ambao si rahisi unaothamini binadamu ili kutimiza lengo la kuwarejesha nyumbani wanajeshi wetu wasiojulikana waliko vilevile walioshiriki katika vita kuilinda nchi yetu ....si jambo rahisi na athari zake ni kubwa.''

Lebanon kwa upande wake inataraji kumpokea Samir Kuntar aliyekuwa jela Israel kwa miaka 29 pamoja na wapiganaji wake wanne Maher Kourani, Khodor Zaidan,
Mohammed Srour and Hussein Suleiman.waliokamatwa wakati wa vita vya Lebanon.Samir Kuntar alikuwa anatumikia kifungo cha maisha baada ya kuwaua Waisraeli wanne mwaka 1979 alipokuwa mwanachama wa kundi la wanamgambo wa KiPalestina.


Hatua hii ya kubadilishana wafungwa inafanyika miaka miwili baada ya pande zote mbili kupigana vita vilivyodumu mwezi mmoja.Israel kadhalika itaikabidhi Lebanon maiti za waarabu 200 waliouawa walipokuwa wakijaribu kuingia eneo la kaskazini.

Shirika la msaada la msalaba mwekundu ICRC linaripotiwa kuchukua jukumu la kufanikisha shughuli hiyo inayotarajiwa kufanyika saa kumi na mbili za London GMT.