1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa ya nje ya Guido Westerwelle

Oumilkher Hamidou29 Septemba 2009

Siasa ya nje inatishia kuzusha mivutano kati ya washirika wa serikali mpya ya nyeusi na manjano

https://p.dw.com/p/JtLa
Mwenyekiti wa chama cha FDP Guido WesterwellePicha: AP

Kiongozi wa chama cha kiliberali cha Free Democratic-FDP-GUIDO WESTERWELLE angependelea sana kufuata nyayo za watangulizi wake na kushikilia wadhifa wa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali ijayo ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na FDP au nyeusi na manjano,kama inavyoitwa.

Katika mada nyingi za siasa ya nje,msimamo wa chama cha kiliberali unalingana na ule wa Christian Democratic CDU.Kwa mfano katika suala la Afghanistan.Kimsingi mkondo uliokua ukifuatwa na muungano wa vyama vikuu ulikua sahihi,anasema kiongozi wa FDP,Guido Westerwelle,akihoji hata hivyo serikali imeshindwa kufanya vya kutosha katika kuijenga upya Afghanistan.Zaidi kuliko yote,mkuu huyo wa chama cha kiliberali cha FDP ameikosoa serikali kwa kutotekeleza ahadi walizotoa za kuimarisha vikosi vya polisi nchi ni humo.

Polisi na wanajeshi wa Afghanistan watakapopata mafunzo ya kutosha ndipo nao wanajeshi wa ISAF wanaoongozwa na NATO watakapoweza kurejea nyumbani.Kuondoshwa kwa pupa wanajeshi wa Ujerumani kutoka Afghanistan kutaitia hatarini Afghanistan na kutishia pia usalama wa Ujerumani.Hapo msimamo wa Westerwelle unalingana na ule wa kansela Angela Merkel.

"Tunataka wanajeshi wetu warejeshwe haraka kutoka Afghanistan,lakini sio bila ya mpango."

Maoni ya washirika katika serikali mpya ya muungano yanatofautiana katika suala la kuwepo wanajeshji wa Ujerumani Bundeswehr nchini Libnan.FDP walipinga bungeni mpango wa kutumwa wanajeshi hao nchini Libnan.Hoja walizotoa ni kwamba wanajeshi wa Ujerumani hawastahiki kuwekwa katika eneo la Mashariki ya kati.Baada ya miaka mitatu ya kuwepo kwa jeshi la wanamaji la Ujerumani katika fukwe za Libnan,mjadala unaweza kuzushwa upya seuze tena wadadisi wanahisi kuwepo kwao huko hakusaidii chochote.

Mada kuhusiana na jeshi la shirikisho Bundeswehr inatazamiwa kugeuka mzizi wa fitina kati ya washirika wa serikali mpya:Chama cha FDP kinataka jukumu la vijana kutumikia jeshi libatilishwe-CDU wanashikilia lakini liendelee."Jukumu la kutumikia jeshi si la haki, na halina maana"walilalamika wana FDP katika kampeni yao ya uchaguzi.FDP wanataka jeshi liundwe kutokana na wanajeshi wanaochagua kufanya kazi hiyo.Kwa hivyo mjadala kuhusu jukumu la kutumikia jeshi,ambao muungano wa vyama vikuu uliuweka kando,unatishia hivi sasa kupamba moto.

Mada nyengine inayozusha mabishano ni kuhusu juhudi za kupunguza silaha.Silaha zilizosalia za atomiki za Marekani zitaondolewa kutoka Ujerumani wakati wa utawala wa serikali mpya-ameahidi Guido Westerwelle kabla ya uchaguzi.Na anapania kuona juhudi za kupunguza silaha zikishikilia mstari wa mbele katika ajenda ya siasa yake ya mambo ya nchi za nje.

Der FDP-Vorsitzende Guido Westerwelle, links, und der frühere Aussenminister Hans-Dietrich Genscher
Guido Westerwelle na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Hans- Dietrich GenscherPicha: AP

Nina Werkhäuser anahisi Guido Westerwelle ana mengi ya kujifunza kutoka kwa watangulizi wake,kuanzia Walter Scheel aliyeshirikiana na msocial Democratic Willy Brandt katika miaka ya 70 kubuni mikataba kuelekea nchi za Mashariki ya ulaya,Hans Dietrich Genscher waziri wa mambo ya nje aliyesalia kwa muda mrefu zaidi madarakani kupita wote humu nchini na aliyechanagia pakubwa katika kuungana upya Ujerumani na Klaus Kinkel aliyekua wa mwanzo kufungua njia ya kutumwa wanajeshi wa Ujerumani nje ya mipaka ya jumuia ya kujihami ya NATO.

Mwandishi:Werkhäuser,Nina/ZR/ Oummilkheir Hamidou

Mhariri:M.Abdul-Rahman