1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za kijani barani Afrika

Kabogo Grace Patricia13 Januari 2010

Chama cha siasa cha Ujerumani kinaonekana kufanya mabadiliko katika uwanja wa kisiasa nchini humo, lakini barani Afrika utunzaji wa mazingira ni kazi ya mashirika ya kiraia.

https://p.dw.com/p/LUzi
Mkuu wa shirika la kimataifa la Greenpeace, Kumi Naidoo.Picha: AP

Wakati chama cha kisiasa cha Ujerumani cha Kijani leo kimefikisha miaka 30 tangu kianzishwe, watu wachache wanatabiri kuwa kitafanya mabadiliko katika uwanja wa siasa za Ujerumani. Lakini kutokana na chama hicho kujihusisha zaidi na masuala ya utunzaji wa mazingira, vyama vyote vilivyoko bungeni vinaliweka suala hilo katika ajenda ya kisiasa, angalau kinadharia.

Vyama vya kijani ama havipo au havina uwezo wowote wa kisiasa. Barani Afrika, kwa mfano utunzaji wa mazingira ni kazi hasa ya mashirika ya kiraia au ya watu wanaojitolea kwa ajili ya kuyatunza mazingira. Kumi Naidoo, mkuu mpya wa shirika la kimataifa la Greenpeace, ni mmoja wa watu wanaojitolea kwa ajili ya kutunza mazingira. Naidoo, aliyezaliwa mwaka 1965 nchini Afrika Kusini, alijiunga na harakati za mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi akiwa na umri wa miaka 15. Katika miaka iliyofuata, alijikuta akitumbukizwa korokoroni kila mara hadi alipoamua kukimbilia uhamishoni. Hivi sasa ulinzi wa mazingira ndio mada kuu anayoipigania. Naidoo anasema barani Ulaya wanaharakati wenzake wa usafi wa mazingira wanaweza kutegemea kuungwa mkono na vyama vya kisiasa. Barani Afrika, hali ni nyengine kabisa.

"Ninadhani katika bara la Afrika fikra ya kuundwa vyama vya kisiasa vya walinzi wa mazingira ni mpya. Tunapolinganisha vyama vya kisiasa vya walinzi wa mazingira barani humo na vile vya Ulaya, ndio kwanza tunaanza. Maarufu zaidi ni vuguvugu la Mkanda wa Kijani-chama kilichoanzishwa na Wangari Maathai wa Kenya miongo kadhaa iliyopita. Kuna vyama chungu nzima vidogo vidogo vya wanaharakati wa usafi wa mazingira pamoja pia na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali-NGOs-yanayoendesha shughuli zao katika kila eneo la Afrika na ambavyo ni muhimu na vyenye kuwazinduwa watu, lakini vinahitaji msukumo ikiwa tunataka kuwa na uwezo wa kukabiliana ipasavyo na changa moto ziliozoko, alisema Naidoo."

Naidoo anasema kuna uhusiano kati ya haki za binaadamu na ulinzi wa mazingira. Katika baadhi ya matukio, umaskini, ukosefu wa ajira na kukiukwa haki za binaadamu ni mambo yanayosababisha uharibifu wa mazingira, kama vile uporaji wa rasilimali za bara hilo. Afrika inasemekana kuwa ni bara linaloathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa. Kuongezeka kwa viwango vya bahari na ukosefu wa mvua, kumesababisha ukame katika maeneo mengi ya Afrika. Naidoo anasema anadhani ujumbe wa mazingira unatakiwa kuwafikia watu wa Afrika, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

''Kama kuna mtu masikini au mtu alieteswa, utaona, utaweza kuelewa na utaguswa. Suala la mabadiliko ya hali ya hewa linalofukuta kidogo kidogo pole pole limekuwa likiendelea kwa muda. Tunaweza tukaufanya ujumbe wa mazingira kuwa maarufu na watu ambao wanapambana na machafuko ya umaskini kila siku, na kwamba kuna uwezekano katika kushughulikia matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa, alisema Naidoo.''

Naidoo anasema anataka kuona watu wanaishi katika dunia yenye usawa kati ya nchi tajiri na masikini, kati ya maisha ya mwanaadamu, maisha ya mimea na wanyama, ambako utunzaji wa misitu siyo tu jukumu la watu wanaopenda misitu, wanaopenda miti, lakini pia ni katika kulinda usalama wa sayari ambapo watu wanaishi.

Mwandishi: Sarah Bomkapre Kamara/Grace Patricia Kabogo/ZR

Mhariri: Miraji Othman