1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea 16 wakiwemo wanawake 2 wanawania kiti cha urais.

Amina Mjahid
8 Machi 2018

Raia milioni 3 wa Sierra Leone wanapiga kura kumchagua rais, wabunge pamoja na machifu. Zoezi hilo lilicheleweshwa kutokana na matatizo ya usajili wa kutumia mfumo wa kielektroniki.

https://p.dw.com/p/2tsv3
Wahlen in Sierra Leone  2018
Picha: DW/A.-B. Jalloh

Katika kituo cha kupigia kura cha Gbense, mjini Koidu baadhi ya wapiga kura wanalalamika kwamba wamepanga foleni ndefu wakisubiri  kupiga kura kuanzia saa sita za usiku lakini vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi ya leo.

"Niliondoka nyumbani kwangu saa kumi na moja asubuhi na nimekuwa hapa muda wote huo nina watoto na ni lazima niwatafutie chakula. siwezi kusimama hapa hadi saa tisa jioni watoto wangu watakula saa ngapi? nataka kupiga kura sasa hivi," alisema mmoja wa wapiga kura

Wahlen in Sierra Leone  2018
Wapiga kura nje ya vituo vya kupigia kura Sierra LeonePicha: DW/A.-B. Jalloh

Mpiga kura mwengine alisema alikuwepo nje ya kituo cha kupigia kura kuanzia saa sita za usiku nililala katika boti lililokuwa karibu. Anasema mambo yanakwenda pole pole sana.

Kwa upande wake afisa anayesimamia kituo hicho cha kupigia kura anakubali kuwa kulikuwa na mkanganyiko na usajili wa wapiga kura hali iliyosababisha kura kuanza kupigwa kuchelewa katika kituo hicho lakini akasema kuwa kwa sasa zoezi hilo linaendelea bila ya wasiwasi wowote.

Takriban watu laki tatu wamejiandikisha  kupiga kura katika wilaya ya Kono yenye utajiri wa almasi. Kono ndio eneo lililo na maendeleo madogo nchini Sierra Leone na wengi wa wapiga kura katika eneo hilo wanatoa wito wa mabadiliko.

Matokeo ya mwanzo kuanza kutolewa saa 48 baada ya zoezi la kupigia kura kukamilika

Mariama Sheriff – Mmoja ya wapiga kura anasema anampigia kura rais wake kwa kuwa ndio kiongozi atakayewaondoa wasierra leone katika mateso wanayopitia. Amesema Kono haina maendeleo na anatumai rais mtarajiwa ataiendeleza wilaya ya Kono kama wanavyotarajia. Ni wazi kwamba raia wengi wanataka mabadiliko na wangelipenda maendeleo katika maeneo wanamoishi lakini likija suala la upigaji kura, kura hizo zinapigwa katika misingi ya vyama .

Wahlen in Sierra Leone  2018
Wapiga kura wakishiriki zoezi la upigaji kura Picha: DW/A.-B. Jalloh

Makamu wa rais wa zamani Samuel Sam Sumana anatokea Kono na anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa. Chama tawala nacho cha All People's Congress APC kilichukua uongozi katika wilaya hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2012 wakati Sam-Sumana alipogombea kupitia tiketi ya chama hicho pamoja na rais Ernest Bai Koroma.

Lakini chama hicho kilipoteza umaarufu wake katika eneo hilo la Kono baada ya rais Koroma kumuondoa Sam-Sumana kama makamu wake. Watu wa Kono wanaendelea kumuunga mkono Sam Sumana lakini nafasi yake ya kushinda ni ndogo kutokana na kukosa umaarufu katika maeneo mengine ya Sierra Leone.

Katika uchaguzi huu wagombea 16 wakiwemo wanawake wawili wanawania kiti cha urais. Mgombea atahitaji kupata asilimia 55 ya kura kushinda duru ya kwanza. Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yanatarajiwa kutolewa saa 48 baada ya zoezi kukamilika huku matokeo kamili yakitarajiwa ndani ya wiki mbili.

Mwandishi: Abu-Bakarr Jalloh /Amina Abubakar

Mhariri:Yusuf Saumu