1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sifa za Rais wa Shirikisho zaingia dowa

Oumilkher Hamidou14 Desemba 2011

Kishindo kinachomkumba rais wa shirikisho Christian Wulff baada ya kuchukua mkopo wa riba nafuu kutoka kwa rafiki yake na vijana na vinywaji vikali ndizo mada zilizomulikwa zaidi magazetini hii leo.

https://p.dw.com/p/13SMt
Rais wa Shirikisho la jamhuri ya Ujerumani, Christian Wulff
Rais wa Shirikisho la jamhuri ya Ujerumani, Christian WulffPicha: dapd

Tuanze lakini na kisa kinachotishia kumharibia sifa yake rais wa shirikisho Christian Wulff.Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika: kwa kusema kila kwa mara sifa za Christian Wulff zinaingia madowa.Kwanza kutokana na kukaa bure katika jumba la fakhari la rafiki yake mmoja ambae ni tajiri, baadae kutokana na kadhia ya Florida na halafu kutokana na kuvutiwa kwake na wote wale waliofanikiwa:matajiri wakubwa wakubwa mfano wa mshauri wa masuala ya fedha Carsten Maschmeyer au huyu wa sasa Egon Geerkens.

Lawama kwamba amelighilibu bunge la jimbo lake ,hazina msingi.Hilo halihusiki lakini na zile hoja kwamba si busara kwa mwenye kudhamini hatamu za uongozi kukubali kuchukua mkopo wa Euro laki tano kwa matumizi ya kibinafsi.Kwasababu mwenye kufadhiliwa hana uhuru seuze tena kama riba ya mkopo wenyewe ni ndogo mno.Wulff hakupima vizuri lakini kisa hicho kiko mbali na kulinganishwa na kashfa.

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine Zeitung" linahisi yadhihirika kana kwamba kuna mtu asiyejifunza kutokana na makosa.Kila wakati Wulff amekuwa akishauriwa ajitenge na wale marafiki ambao kwakuwa karibu nao anaweza kutiliwa dhana.Wengi wa wajerumani wanaweza kumsamehe makosa yake Christian Wulff-kwa sharti lakini kwamba cha kusamehewa kinajulikana na sio kila siku mepya yanachomoza.

Mjasiriamali Egon Geerkens
Mjasiriamali Egon GeerkensPicha: picture alliance/dpa

Ni bahati yake Wulff kwamba sifa yake haijachujuka.Wengi nchini Ujerumani bado wanaikumbuka hotuba aliyoitoa kuhusu juhudi za kujumuishwa wageni katika maisha ya kijamii humu nchini.Na hata katika nchi za nje Christian Wulff anajivunia sifa-nchini Poland na Israel ambako rais huyo mpya wa shirikisho anaangaliwa kuwa ni rafiki wa kutegemewa.

Mada yetu ya pili inahusika na vijana na vinjwaji vikali.Gazeti la "Donaukurier" linasema baadhi ya matatizo hayamaliziki hivi hivi.Ingawa si mara nyingi kuwaona watoto wanapelekwa hospitali kwasababu ya sumu ya ulevi,lakini hiyo si sababu ya kupumua-kama ilivyodhihirika katika ripoti iliyochapishwa hivi karibu na idara kuu ya takwimu ya humu nchini.Kunywa ulevi mpaka wakazimia ndio mtindo unaozidi kupendwa na vijana-ripoti hiyo imesema. Yadhihirika kana kwamba vijana wengi bado wako mbali na kunywa kwa starehe sawa na chama cha FDP kilivyo mbali na kujipatia imani ya walio wengi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-Rahman