1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sigmar Gabriel achaguliwa upya kuiongoza SPD

15 Novemba 2013

Mkutano mkuu wa dharura wa chama cha Social Democratic, SPD, unaendelea mjini Leipizig. Sigmar Gabriel amechaguliwa upya kukiongoza chama hicho lakini hakupata kura nyingi ikilinganishwa na miaka 4 iliyopita.

https://p.dw.com/p/1AIAG
Mwenyekiti wa chama cha Social Democratic, SPD, Sigmar GabrielPicha: Reuters

Mkutano huo mkuu wa dharura wa chama cha Social Democratic unafanyika katika wakati ambapo mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano kati ya vyama ndugu vya Christian Democratic Union,CDU, Christian Social Union, CSU na Social Democratic, SPD, yameshika kasi. Katika zoezi la upigaji kura, mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel, amejikingia asilimia 83.6 tu ya kura safari hii - Ni haba ikilinganishwa na asilimia 94.2 alizopata alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2009 au asilimia 91.8 alizojikingia miaka miwili baadaye.

Hata hivyo Sigmar Gabriel amewashukuru wajumbe mkutanoni kwa kile alichokiita "matokeo ya dhati ya uchaguzi katika wakati huu wa kipekee." Hapo alikuwa akigusia wakati huu ambapo mkutano wa kuunda serikali kuu ya muungano unaendelea huku SPD wakishinikizwa na wanachama wake wanaotaka kuona madai yao muhimu yanazingatiwa.

SPD Parteitag 14.11.2013
Wajumbe katika mkutano mkuu wa chama cha SPD mjini LeipzigPicha: Johannes Eisele/AFP/Getty Images

Hakuna Muungano bila ya madai kuzingatiwa

Ili kutuliza hofu za wanachama, mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel amesema, "Hatutofuata kwa mara ya pili mkondo wa siasa ambayo SPD kwa mara nyengine tena itakiuka muongozo wake. Ndio maana mshahara wa chini wa Euro 8.5 kwa saa kwa wote, lazima ukubaliwe, bila ya hilo hakuna muungano utakaofanyika pamoja na SPD."

Gabriel ameutaja ushirikiano pamoja na muungano wa CDU-CSU kuwa ni ushirikiano wa busara na wa muda. Anasema juhudi za kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi na kupigania uraia wa nchi mbili ni juhudi za maana zinazostahiki kupiganiwa katika mazungumzo hayo ya kuunda serikali ya muungano. Miito imehanikiza pia katika mkutano huo mkuu mjini Leipzig kutaka chama cha SPD kifanyiwe mageuzi yanayoambatana na wakati.

SPD Parteitag 14.11.2013 Andrea Nahles
Katibu mkuu wa chama cha SPD, bi Andrea NahlesPicha: Reuters

SPD chawachagua viongozi wake

Baadaye hii leo uongozi jumla wa chama wakiwemo katibu mkuu, Andrea Nahles, na makamo wenyeviti, Hannelore Kraft, Aydan Özguz, Olaf Scholz na Manuela Schwesig, watapigania upya nyadhifa zao. Nafasi ya meya wa jiji la Berlin, Klaus Wowereit, aliyeamua kutopigania tena wadhifa wake chamani, itagombewa na mwenyekiti wa chama cha SPD katika jimbo la Hessen, Thorsten Schäfer-Gümbel.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri: Josephat Charo