1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Kimataifa Kupinga Adhabu ya Kifo

P.Martin10 Oktoba 2007

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Lisbon nchini Ureno,wanahimiza kuimarisha juhudi za kidiplomasia ili kupiga marufuku adhabu ya kifo kila pembe ya dunia.Hii leo,kwa mara ya kwanza inaadhimishwa siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani.

https://p.dw.com/p/C77v

Oktoba 10 imeshapangwa kama ni siku ya kupinga adhabu ya kifo kote duniani,sasa kuna haja gani ya kuitisha mkutano wa Lisbon kuhakikisha siku hiyo,mkutano ambao unagharimu pesa nyingi mno? Hilo bila shaka ni suala linaloulizwa na wakosoaji na wapinzani wa kampeni ya kupiga marufuku adhabu ya kifo.

Hata hivyo,tangu miongo kadhaa idadi ya nchi zinazopiga marufuku adhabu ya kifo imeongezeka. Kwa mfano katika mwaka 1976 nchi 16 tu zilifuta adhabu ya kifo,lakini hii leo nchi 133 ama zimeondosha kabisa au kisheria,zimepiga marufuku adhabu hiyo.Miongoni mwa nchi hizo 91 zimefuta kabisa adhabu ya kifo.Wakati huo huo katika nchi 64 bado adhabu ya kifo inaendelea kutumika. Takwimu zinaonyesha kuwa tangu miaka na miaka, China,Iran,Pakistan,Irak,Sudan na Marekani zinatia fora kutekeleza adhabu ya kifo.

Baraza la Ulaya limeweka sharti kuwa nchi inayotaka kuwa mwanachama inapaswa kuondosha adhabu ya kifo.Kwa hivyo,nchi 47 wanachama na wakaazi wake milioni 800 wametia maanani haki ya kimsingi ya binadamu.Hiyo pia ni sababu zaidi kwa Ulaya kugombea kupinga adhabu ya kifo kila pembe ya dunia.Wito wa kuzia adhabu ya kifo, umefungamana na haki za binadamu na hauwezi kutenganishwa.Vile vile,kuhifadhiwa haki za binadamu ni mwongozo wa Ulaya ulioandikwa kwenye bendera.

Taifa linaloua kwa niaba ya umma na kwa hivyo kwa niaba ya raia wote,hujifanya kuwa muuaji.Adhabu ya kifo ni kitendo cha kinyama kisichomsaidia muhanga aliefanyiwa uhalifu wala haisaidii kuzuia uhalifu.Kinyume na hayo,panapotokea kosa la mahakama na adhabu ya kifo kutekelezwa,kosa hilo halitoweza kurekebishwa na huwa aibu ya jumuiya nzima.

Ikiwa mwongozo wa jamii ni kulipiza kisasi yaani „Jicho kwa jicho“,matokeo yake hayatokuwa na haki.Ujumbe wa Ulaya,bara lililojifunza kutokana na historia yake ya umwagaji damu ni huu: anaepanda mbegu ya kifo atavuna kifo.